WAZIRI AWESO ABAINISHA MIKAKATI KUKABILIANA NA CHANGAMOTO YA MAJI DAR, PWANI
Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso ameeleza mipango mbalimbali inayofanywa na Serikali katika kuboresha huduma ya maji katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Mheshimiwa Aweso ameainisha mipango hiyo akizungumzia katika kipindi Cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC).
"Moja ya mipango itakayomaliza changamoto ya maji katika mikoa hii ni ukamilishaji wa Bwawa la Kidunda, lakini pia tunaendelea na mpango wa kuongeza uwezo wa uzalishaji katika mtambo wa Ruvu chini, zaidi tuna mitambo ya uchimbaji visima maeneo mbalimbali visima ambavyo vitapunguza adha ya maji, lakini pia tunaenda kuanza awamu ya pili ya visima vya Kimbiji Kigamboni ili kutatua adha ya maji," amesema Mheshimiwa Aweso.
Aweso amesema Serikali imekwishaanza utekelezaji wa Gridi ya Taifa ya maji ambapo vyanzo vikuu vya maji nchini vitaunganishwa ili kuhudumia wananchi.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire amesema jitihada kubwa zinaendelea katika ufuatiliaji wa ratiba ya mgao wa maji inayoendelea ili kuhakikisha kila mwananchi anapata maji.
"Tunaendelea kutoa elimu pia kwa wananchi ni siku gani wanapata huduma ya maji ndani ya wiki, hii inasaidia kumpatia muda wa kujiandaa na kupata huduma hiyo katika siku husika," amesama Mhandisi Bwire.
Bwire amesema DAWASA inatambua kuna changamoto zinajitokeza wakati wa mgao pengine maji kushindwa kufika katika baadhi ya nyumba, lakini timu za ufundi zipo mtaani kutatua changamoto hizo mapema zinapojitokeza.
