Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YATATUA CHANGAMOTO YA MAJI MTAA WA MUUNGANO - GOBA
20 Nov, 2024
DAWASA YATATUA CHANGAMOTO YA MAJI MTAA WA MUUNGANO - GOBA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) inaendelea na utekelezaji wa mradi wa kuimarisha huduma ya majisafi katika Mtaa wa Muungano Kata ya Goba, Wilaya ya Ubungo.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa Mkoa wa kihuduma DAWASA Mivumoni Ndugu, Gilbert Masawe amewatoa hofu wakazi wa mtaa wa Muungano hususani wa eneo la Marobo kuwa, baada ya kukamilika kwa mradi huu huduma ya maji itaimarika na kila mwananchi atapata Maji ya kutosha. 

"Mradi huu unahusisha uchimbaji na ulazaji wa bomba za ukubwa wa inchi 8 kwa umbali wa kilomita 1.5, tunategemea mradi utakamilika mapema wiki ijayo na wananchi wa Marobo watapata huduma bora ya majisafi," ameeleza Ndugu Masawe.

Masawe ameongeza kuwa lengo la mradi huu ni kuongeza msukumo wa maji kwa wananchi ambao walikua wanapata huduma kwa kusuasua na kupelekea Mamlaka kuja na mradi huu unaoenda kuwa suluhisho la kudumu katika eneo la Marobo. 

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Muungano Ndugu Godwin Mangowi, ameishukuru Serikali kupitia DAWASA kwa kuja na mradi huu katika mtaa anaousimamia kwani utajibu changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji eneo la Marobo. 

"Shukrani zangu kwa Serikali ya Awamu ya Sita kupitia DAWASA kwa kutekeleza mradi huu muhimu sana katika mtaa wa Muungano, hususani eneo la Marobo, wananchi walikua wanakosa huduma ya maji hadi wiki tatu lakini tunaimani sasa kero hiyo inakwenda kumalizika," ameeleza Ndugu Mangowi