DAWASA YATETA NA WAJUMBE WA MASHINA KINONDONI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imekutana na Wenyeviti wa mitaa na Wajumbe wa mashina katika kata ya Msasani kutoka mitaa ya Bonde la Mpunga, Makangira, Masaki, Mikoroshini na Oysterbay kwa lengo la kutoa elimu kuhusu huduma zinazotolewa na DAWASA pamoja na kuweka mikakati ya pamoja katika kupambana na upotevu wa maji.
Akiongea na viongozi hao, Meneja wa DAWASA Mkoa wa kihuduma Kinondoni, Tumaini Muhondwa amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Mamlaka na jamii ili kufanikisha malengo ya upatikanaji wa majisafi na salama haswa katika mitaa hiyo.
“Wilaya ya Kinondoni kuna changamoto ya upotevu wa maji, tunaamini kwa kushirikiana na wenyeviti wa mitaa na wajumbe wa mashina, tunaweza kupunguza upotevu wa maji kwa njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu, kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi bora ya maji, na kubaini maeneo yanayokumbwa na upotevu mkubwa,” amesema Muhondwa
Ndugu Muhondwa amesema kwa kuanza ushirikiano wa karibu, wameweka utaratibu wa kutambulisha watendaji wa DAWASA kwa wajumbe wa mashina hadi wenyeviti wa serikali za mitaa ili kurahisisha ushughulikiwaji wa changamoto na taarifa zinazotolewa na wateja.
Ndugu Atanas Michael, mjumbe wa Shina kutoka Serikali ya mtaa Bonde la mpunga ameishukuru DAWASA kwa elimu iliyotolewa na kuhakikisha kuwa balozi mzuri kwa wananchi ndani ya eneo lake.
"Tunapongeza DAWASA kwa ushirikishwaji huu, tumepokea elimu ambayo hatukuwa nayo. Tunaahidi kuendelea kushirikiana na DAWASA katika utoaji wa huduma pamoja na utekelezaji wa shughuli katika maeneo yetu." ameeleza ndugu Michael