DAWASA YATETA NA WAKAZI MKURANGA - ELIMU KWA UMMA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imekutana na kuwakumbusha wateja wa mji wa Mkuranga umuhimu wa kulipa bili za maji kwa wakati ili kuiwezesha Mamlaka kuendelea kutekeleza shughuli ya kusambaza zaidi huduma ya maji kwa wananchi.
Hayo yameelezwa na afisa huduma kwa wateja DAWASA-Mkuranga Ndugu Sufian Hassan wakati wa kikao na wananchi kilichoajadili uimarishaji huduma za Maji.
Amesisitiza ulipaji wa bili za maji hususani kwa wananchi wenye malimbikizo ya madeni ya maunganisho ya maji.
Ndugu Sufian amesisitiza wananchi kuendelea kutumia huduma ya DAWASA na kuacha matumizi ya maji yasiyo rasmi kwa kuwa maji yanayotolewa na Mamlaka yamepimwa na kukidhi viwango vya ubora wa kimataifa kwa matumizi ya afya ya binadamu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkuranga , Ndugu Dunia Mabuyu amewasisitiza wananchi kuwafichua watu wanaohujumu miundombinu ya DAWASA kwani wizi wa miundombinu ya maji umeshamiri kwa eneo la Mkuranga.
"Vitendo vya wizi wa miundombinu ya maji havikubaliki maana vinafifisha jitihada za Serikali za kutoa huduma kwa wateja na kwa ufanisi, ni vyema kila mwananchi awe mlinzi wa miundombinu hii kwa manufaa yetu na vizazi vijavyo." ameeleza Ndugu Mabuyu.
Mkazi wa Mkuranga, Yahaya Mwendapole ameiomba Mamlaka kuongeza bidii ya kusambaza huduma ya maji kwa wananchi wote ili kila mmoja anufaike na kazi kubwa ya Serikali.
"Pia kwa maeneo ambayo huduma haifiki, Mamlaka ijitahidi kuongeza nguvu kusogeza huduma ili iwafikie wananchi wote," ameeleza Ndugu Mwendapole.