DAWASA YATINGA BUGURUNI KISIWANI UBORESHAJI MIUNDOMBINU YA MAJITAKA

Yatoa rai ulinzi na utunzaji miundombinu
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imetekeleza zoezi la uboreshaji wa miundombinu ya majitaka katika mtaa wa Buguruni Kisiwani, Wilaya ya Ilala ikiwa na lengo la kuongeza ufanisi pamoja na kuondoa uwezekano wa magonjwa ya milipuko.
Maboresho hayo yamefanywa kwa lengo la kuondoa changamoto ya uvujaji na utiririshaji wa majitaka katika mtandao wa bomba unaosafirisha majitaka kutoka katika makazi yq watu hadi mabwawa ya majitaka Buguruni.
Akieleza maboresho hayo, Mhandisi Gabriel Wanzagi amesema kuwa DAWASA inaendelea na uboreshaji wa mtandao wa majitaka eneo la Buguruni Kisiwani unaohussish uondoshaji wa majitaka, usafi wa chemba pamoja na kubadilisha miundombinu chakavu ikiwemo kubadilisha bomba kwa umbali wa mita 40.
"Sambamba na kazi zinazoendelea, nipongeze ushirikiano mzuri kutoka kwa Wananchi ambao wamekuwa ni wepesi kututafuta pale wanapoona changamoto. Tuwasihi waendelee kuwa mabalozi wazuri wa kutunza miundombinu kwa kuepuka kutupa taka ngumu katika miundombinu ya Maji ili kuepuka athari mbalimbali pindi miundombinu hiyo inaposhindwa kupitisha Majitaka." ameeleza
Mjumbe wa kamati ya Mazingira mtaa wa Buguruni Kisiwani, Bi Kuruthum Omar ameshukuru jitihada zilizofanywa na DAWASA za kusafisha miundombinu ya majitaka na kuleta ahueni kwa wakazi wa maeneo hayo ambapo ametoa rai kwa Mamlaka kuendelea kushirikiana na wananchi ili kuilinda miundombinu ya kuondosha majitaka.