Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YATOA ELIMU UTUNZAJI WA MIUNDOMBINU KIBASILA
16 Oct, 2025
DAWASA YATOA ELIMU UTUNZAJI WA MIUNDOMBINU KIBASILA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetoa elimu ya umuhimu wa maji na utunzaji miundombinu ya maji kwa wanafunzi wa klabu ya mazingira shule ya sekondari Kibasila, Wilaya ya Temeke Mkoani Dar es salaam.

Lengo la elimu hii ilikuwa ni  kuwaelemisha wanafunzi umuhimu wa maji na utunzaji wa miundombinu ya maji ili waweze kuwa mabalozi wazuri wa huduma hii muhimu katika jamii.

Akizungumza wakati wa kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule hiyo, Afisa Mawasiliano kutoka DAWASA, Ndugu Prisca Makenya amesema maji ni rasilimali  muhimu ambayo inahitajika kwa viumbe hai ikiwepo binadamu, mimea na wanyama, hivyo kuna ulazima wa kuyatunza na kuhakikisha yanalindwa ili yaweze kufaa kwa matumizi ya kila siku.

"Utunzaji miundombinu ya maji ni muhimu kwani unapunguza gharama zinazojitokeza wakati wa uharibifu, unasaidia upatikanaji majisafi na ya  uhakika. 

Miundombinu ya maji inayotumiwa na  DAWASA ni pamoja na  mitambo ya uzalishaji  na Uzalishaji maji, mabomba, pumpu za kusukuma maji, dira za maji na viungio vyake," amesema Ndugu Makenya.

Ndugu Makenya amesema klabu za mazingira mashuleni zimeanzishwa kwa lengo la kuwajengea vijana uwezo katika masuala ya maji na usafi wa mazingira ili wanafunzi hao wakawe chachu na mabalozi wa mabadiliko kwa jamii wanazotoka. 

Wanafunzi wamejifunza njia mbalimbali ovu zinazofanywa na wanachi wasiowaaminifu kwenye  miundombinu ya DAWASA ikiwa ni pamoja na kukata mabomba, wizi wa mita za maji, kurudisha usomwaji wa mita nyuma. 

Kwa upande wake, Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Kibasila,  Emmanuel Sedekia ameishukuru Mamlaka kwa kutoa elimu hii muhimu kwa wanafunzi wa shule hiyo inayowajengea uelewa wa namma nzuri ya kutunza miundombinu ya maji na hatua za kuchukua punde wanapoona wananchi wasio waaminifu wanaoharibu miundombinu.

Amewataka wanafunzi waliopatiwa elimu hiyo kuwa mabalozi wazuri wa huduma za maji katika jamii yao. 

Mwanafunzi, Mashiri Bozuga aliyepata elimu hiyo, ameishukuru Mamlaka kwa kuwaelimisha na kuwasaidia kujua umuhimu wa utunzaji wa miundombinu ya maji na hatua za kuchukua pindi wanapoona uharibifu unapotokea,  ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa DAWASA kupitia namba  181 ya huduma kwa wateja.

"Kwa niaba ya wenzangu, tunaahidi tutakuwa mabalozi wazuri kwa jamii kuhakikisha tunalinda miundombinu ya maji kwa manufaa ya vizazi vijavyo," amesema Buzuga.

Klabu ya Mazingira Shule ya Kibasila ni moja ya klabu 11 za mazingira ambazo Mamlaka inazisimamia katika Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani ili kuwajengea uwezo wa kutambua shughuli mbalimbali za Mamlaka kuhusu majisafi na usafi wa mazingira na kwenda kuwa mabalozi wazuri katika jamii.