DAWASA YATOA MADINI KWA WANAFUNZI WA SHULE YA OYSTERBAY

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetoa elimu ya ujuzi wa namna bora na ya kisasa ya kuboresha Usafi wa Mazingira kwa Wanafunzi wa Shule ya Msingi Oysterbay ili waweze kuwa mabalozi na wataalam wazuri.
Shule ya Oysterbay ni miongoni mwa shule 10 za Mazingira zinazosimamiwa na kuendeshwa na DAWASA.
Afisa Mawasiliano kutoka DAWASA Bi. Hashura Kamugisha ameeleza kuwa shughuli (tabia) mbalimbali zinazochangia uharibifu wa miundombinu na mifumo ya majitaka pamoja na athari zinazoweza kutokea pale miundombinu ya majitaka inapokuwa imeharibiwa katika maeneo yao.
"Miundombinu ya Majitaka isipotunzwa na kutumika kwa usahihi inasababisha madhara mengi ndani ya jamii ikiwa ni pamoja na kuziba kwa chemba na mifumo ya maji taka jambo ambalo hupelekea uharibifu wa mazingira na mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza, hivyo ni jukumu la kila mmoja kutunza miundombinu hiyo iliyopo katika maeneo yenu mnayoishi," ameeleza Ndugu Kamugisha.
Nae Mwalimu Nina Jeremani mlezi wa klabu ya mazingira shuleni hapo ameishukuru Mamlaka kwa jitihada za kutoa elimu ya utunzaji Mazingira kwa ujumla na kusisitiza kuwa wanafunzi wanatakiwa kuwa mabalozi wenu kuifikisha elimu hii kwa wanafunzi wenzao na jamii wanayoishi.
"Elimu ya utunzaji wa Mazingira hasa Majitaka imekuja kwa wakati sahihi na kwa watu sahihi na ni elimu inayopaswa kurithishwa kwa watu wa rika zote, kwa kuanzia na hawa wanafunzi wadogo kunawasaidia kujijengea tabia endelevu na kuchukua majukumu ya utunzaji wa Mazingira. Muwe mabalozi wema katika kutumia vizuri vyoo kwa kutotupa taka ngumu mkiwa nyumbani au hata shuleni," ameeleza Mwl. Nana.
Mwanafunzi Jamaldini Abasi ambae ni mwanachama wa klabu ya maji na usafi wa Mazingira ya shule ya msingi Oysterbay ameishukuru DAWASA kwa kuwa mlezi na kutoa nafasi ya wao kujifunza mambo mbalimbali ya Maji na Usafi wa Mazingira na kuomba nafasi ya kuendelea kujifunza kwa vitendo ili kufahamu zaidi namna Mamlaka inavyoendesha shughuli zake.
Kwa kupitia DAWASA tumeweza kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu Mazingira na maji, na leo tumejifunza somo la Majitaka ambalo kwa rika letu ni somo la msingi kwani limetujengea uelewa zaidi juu ya matumizi sahihi ya miundombinu ya Majitaka ili kuendelea kutunza mazingira na kujiepusha na magonjwa mbalimbali.