DAWASA YAUKATA UPEPO CRDB MARATHON

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) wameungana na taasisi za umma, mashirika binafsi pamoja na wananchi mbalimbali katika mbio za CRDB Marathon zilizofanyika leo Jumapili, Agosti 17, 2025 jijini Dar es Salaam.
Lengo mbio hizo ambazo mgeni rasmi alikuwa Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Mabunge Duniani (IPU) ni kukusanya fedha kusaidia watoto wenye matatizo ya moyo, yatima na familia zisizojiweza.
Akizungumzia kwaniaba ya washiriki wote kutoka DAWASA, Mkuu wa Kitengo cha Mazingira, Mhandisi Modesta Mushi amesema umuhimu wa kushiriki mbio hizo huku akielezea umuhimu wa mazoezi kwa watumishi wote.
"Kwanza nichukue fursa kumshukuru Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Mhandisi Mkama Bwire kwa kuruhusu kushiriki katika mbio hizi muhimu.
Kama taasisi tunayohudumia wananchi imekuwa vyema kuungana na wenzetu katika kutimiza lengo la kusaidia jamii yenye uhitaji kwa kuchangia matibabu ya moyo, yatima pamoja na familia zisizojiweza kupitia mbio hizi," amesema Mhandisi Mushi
Mhandisi Mushi amesema uwepo wa DAWASA kushiriki mbio hizi za CRDB Marathon ni chachu kwa watumishi wote kuendelea kupenda mazoezi binafsi na kuimarisha afya zao ili kuupa mwili utayari wa kuhudumia wananchi wakati wowote.
Mbio za CRDB International Marathon kwa mwaka 2025 zimebeba kauli mbiu isemayo "Kasi isambazayo Tabasamu."