DAWASA YAWAHIMIZA WATEJA TEMEKE KUKAMILISHA MALIPO YA HUDUMA ZA MAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kupitia Mkoa wa kihuduma Temeke imewahimiza Wakazi na Wananchi wanaohudumiwa na Mamlaka kulipa bili za mwezi kwa wakati ili kuwezesha Mamlaka kuboresha zaidi huduma zake.
Afisa Biashara DAWASA Temeke, Ndugu Hassan Kapambala amesema kuwa kupitia Mkataba wa huduma kwa wateja umeainisha kuwa mteja anao wajibu wa kulipia ankara yake ya Maji kwa wakati kulingana na matumizi yake ya mwezi husika.
"DAWASA imeweka dhamira ya kufikisha huduma kwa wateja wote kwa ubora. Hivyo ni vyema wananchi wakafahamu kuwa Mamlaka inategemea makusanyo ili kutekeleza miradi ya usambazaji maji pamoja na kuendelea kuwahudumia wananchi" amesema.
Ndugu Hassan amesema kuwa zoezi la ufuatiliaji wateja wenye madeni nyumba kwa nyumba linaendelea katika maeneo mbalimbali ndani ya eneo letu la kihuduma.
"Tunawasisitiza wateja wote wawe na utamaduni wa kulipa bili zao bila kulaza deni ili waweze kumaliza mwezi huu bila deni lolote la maji kutoka kwetu," ameeleza.
Mkoa wa kihuduma DAWASA - Temeke unahudumia wateja takribani 15,686 katika kata 18 za Kivule, Mzinga, Kitunda, Minazi mirefu, Kiwalani, Makangarawe, Kilakala, Buza, Yombo Vituka, Mtoni, Miburani, Tandika, Sandali, Kurasini, Azimio, Keko na Temeke.