Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAWAINUA WAKAZI WA BOKO DOVYA - MAPOKEZI UPATIKANAJI HUDUMA YA MAJI
11 Feb, 2025
DAWASA YAWAINUA WAKAZI WA BOKO DOVYA - MAPOKEZI UPATIKANAJI HUDUMA YA MAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inaendelea kuwafikia wananchi na kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia suluhisho kupitia kampeni yake ya DAWASA Mtaa kwa Mtaa, ambapo kupitia jitihada hizi, wakazi 420 wa Mtaa wa Boko Dovya Mapokezi, Kata ya Bunju, Wilaya ya Kinondoni, wamepewa uhakika wa upatikanaji wa huduma ya majisafi kupitia mradi mpya wa maji wa Dovya Mapokezi.  

Mradi huu unahusisha ulazaji wa mabomba ya inchi 4 kwa umbali wa mita 450, hatua inayolenga kupunguza changamoto ya msukumo mdogo wa maji na kutatua tatizo la ukosefu wa maji katika eneo hilo. 

Akizungumza wakati wa ziara fupi katika eneo hilo, Mkurugenzi wa Fedha wa DAWASA, Ndugu Sais Kyejo, alieleza dhamira ya Mamlaka kuhakikisha huduma ya majisafi inawafikia wananchi kwa haraka. 

Amesema kuwa kukamilika kwa mradi huu kutawanufaisha wakazi wa eneo hilo pamoja na taasisi muhimu kama Boko Magereza, Shule ya Sekondari Boko, Shule ya Msingi Boko, na Kituo cha Polisi Boko.

Ndugu Kyejo amebainisha kuwa moja ya changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa mradi huu ni ugumu wa ardhi inayochimbwa kwa ajili ya kulaza mabomba.

“Mamlaka iko kazini kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa wakati, kwani ndicho kipaumbele chetu cha kwanza. Uchimbaji wa mabomba umekumbwa na changamoto kutokana na uwepo wa miamba ya kokoto katika eneo hili. Hata hivyo, tumepanga kutumia vifaa vyenye uwezo mkubwa ili kurahisisha na kuharakisha kazi hii," amesema Ndugu Kyejo. 

'Tunawaomba wananchi wawe na subira kwani tupo kazini usiku na mchana kuhakikisha huduma hii inapatikana,” alisema Bw. Kyejo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maji na Mazingira, Ndugu Peter Hanosi Mdamwa, ameishukuru DAWASA kwa jitihada zake na kwa ushirikiano mzuri na wananchi.

“Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya kuhakikisha tunapata huduma ya maji. Jambo kubwa zaidi ni kuwashukuru kwa kuwa wasikivu na kutushirikisha sisi viongozi wa Serikali ya mtaa katika mipango yenu. Ushirikiano huu unatusaidia kuwaelimisha wananchi kuhusu kinachoendelea. Tuna matumaini kuwa mradi huu utakamilika kwa haraka kwa kuwa uhitaji wa maji ni mkubwa,” alisema Ndugu Peter.

Wananchi wa Boko Dovya Mapokezi wamefurahia kuona DAWASA inawatembelea na kusikiliza changamoto zao, huku wakionesha matumaini kuwa kilio chao kinasikilizwa na kufanyiwa kazi.

“Kuwaona hapa leo kumetupa faraja kubwa. Tumekuwa na changamoto ya maji kwa muda mrefu, hivyo tunawashukuru sana DAWASA kwa kutusikiliza. Tunawaomba muongeze juhudi kukamilisha mradi huu na pia kutupelekea mabomba katika maeneo ya bondeni ili wote tufaidike na huduma hii muhimu,” alisema Bi. Beatrice John, mkazi wa Dovya Mapokezi.

DAWASA inaendelea na juhudi zake za kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa wananchi wake. Aidha, Mamlaka inawashirikisha wananchi kwa njia mbalimbali, ikiwemo kampeni za Nyumba kwa Nyumba, mikutano ya hadhara, na mitandao ya kijamii, ili kuhakikisha wanatambua juhudi zinazoendelea katika kuboresha huduma za maji jijini Dar es Salaam.