DAWASA YAWANOA MABALOZI WA MAJI CHALINZE
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetoa elimu ya utunzaji wa majisafi kwa shule ya Sekondari Chalinze, Mkoa wa Pwani.
Lengo ni kuwaelimisha wanafunzi kuhusu umuhimu wa majisafi na usafi mazingira ili waweze kuwa mabalozi kwa jamii yao.
Klabu ya mazingira iliyopo shule ya Chalinze ni mojawapo ya klabu 11 ambazo Mamlaka inazisimamia kwa lengo la kujenga uelewa kwa wanafunzi kuhusu umuhimu wa majisafi na usafi wa mazingira.
Akizungumza wakati wa kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule hiyo, Afisa Mawasiliano kutoka DAWASA, Bi Prisca Makenya amesema maji ni rasilimali muhimu ambayo inahitajika kwa viumbe hai ( binadamu na wanyama), hivyo kuna ulazima wa kuyatunza na kuhakikisha yanalindwa ili yaweze kufaa kwa matumizi ya kila siku.
Amesema Mamlaka imetoa elimu juu ya matumizi sahihi ya maji ili kupunguza matumizi makubwa yasiyo ya lazima ya maji hasa wakati wa kunawa mikono kwa vitendo katika mazingira yao ya shule, pamoja na kuwasisitiza wazazi nyumbani kuwa na vyombo ziada vya kuhifadhi maji kama vile ndoo, matenki, kutotumia maji moja kwa moja kutoka bombani wakati wa kuosha vyombo, kufua na wakati wa kunawa.
Amesema klabu za mazingira mashuleni zimeanzishwa kwa lengo la kuwajengea vijana uwezo katika masuala ya maji na usafi wa mazingira ili wanafunzi hao wakawe chachu na mabalozi wa mabadiliko kwa jamii wanazotoka na wanafunzi wenzao.
Kwa kupitia makundi yao yaliyoundwa wakati wa kipindi, wanafunzi wameweza kujadiliana na kukubaliana ustawi wa jamii yoyote ile unategemea huduma ya majisafi na salama kwa upatikanaji wa maji salama utasaidia katika usafi wa mwili na mazingira, lakini pia kupunguza magonjwa katika jamii na maji hutumika katika shughul mbali mbali za kibinadamu kama vile kilimo na biashara.
Wanafunzi wa Klabu ya mazingira pia wameelekezwa juu ya vyanzo vya maji na umuhimu wa kulinda na kutunza vyanzo hivyo.
Katika hatua hiyo, wanafunzi wamejifunza njia mbalimbali ambazo jamii inaweza kutumia kulinda vyanzo vya maji kama vile kutofanya shughuli za uharibifu wa mazingira karibu na vyanzo vya maji, kutokata miti ovyo karibu na vyanzo vya maji, kupanda miti na kutokutupa taka ngumu ovyo katika au karibu na vyanzo vya maji.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Shule ya Sekondari Chalinze, Filemoni Hechei ameishukuru Mamlaka kwa kutoa elimu hii muhimu kwa wanafunzi wa shule hiyo inayowajengea uelewa wa nama nzuri ya kutunza maji na kuwa mabalozi wazuri wa maji katika jamii yao.
Amewataka wanafunzi kuondoka na elimu hiyo kichwani na kwenda kuitumia kuwaelimisha watu wa nyumbani kwa lengo la kuepuka matumizi yasiyo ya lazima ya maji yanayopelekea kulipa gharama kubwa ya maji.
Naye mwanafunzi, Elizabeth Hanu aliyepata elimu hiyo aliishukuru DAWASA kwa kuwaelimisha na kuwasaidia kujua namna bora ya kutumia maji ili kuepuka matumizi mabaya ya maji.
Pia, ameshukuru kwa kuelewa umuhimu wa kutunza miundombinu ya maji na kuahidi kuwa balozi mzuri wa maji kwa watu anaoishi nao.
