DAWASA YAWAPA RUNGU VIONGOZI MAKURUNGE KUWABAINI ‘WALAGHAI’ WA HUDUMA
Kufuatia kujitokeza kwa wingi kwa vitendo vya ulaghai wa Watu wachache wanaowarubuni Wananchi kutoa fedha ili waunganishiwe huduma ya Maji katika Kitongoji cha Makurunge, Kata ya Kiluvya Mkoani Pwani, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imeweka mikakati ya pamoja na Viongozi wa Serikali za mitaa kutoka mashina 25.
Mikakati hiyo ya pamoja imewekwa kupitia kikao kazi cha DAWASA na watendaji wa Makurunge kilicholenga kuweka mikakati ya uboreshaji huduma ya maji katika eneo hilo na kusikiliza changamoto za huduma.
Akizungumzia katika kikao kazi hicho Mwenyekiti wa mtaa wa Makurunge ndugu, Peter John Mgeni ameeleza kuwa changamoto kubwa ya huduma ya maji inayojitokeza katika eneo hilo ni ongezeko la Watu na shughuli za kiuchumi sambamba na Vishoka wachache wanaopita kuwahadaa Wananchi kiasi cha fedha ili waunganishiwe Maji kinyume na utaratibu wa DAWASA.
“Tumebaini uwepo wa walaghai wachache wanaopita katika Kitongoji chetu kuwadanganya Wanachi kuwa watoe fedha cash ili waunganishiwe huduma. Tumeazimia kufanya msako wa kuwabaini pamoja na DAWASA ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizi” alisema Mgeni
Mgeni ameongeza kuwa katika mashina 25 ya Kitongoji bado uhitaji wa huduma ya Maji ni mkubwa na sehemu nyingine hawapati huduma ya majisafi na wengine wakipata huduma ya maji kwa msukumo mdogo.
"Wananchi wa Makurunge wanahitaji huduma ya maji na wananchi hawa wapo tayari kushirikiana na DAWASA kwa kila hali Ili huduma ya maji iwafikie, Kuna maeneo ambayo mtandao umeshapita ila Wananchi wanahitaji kupimiwa na kuunganishwa na huduma. DAWASA iharakishe mchakato ili kutotoa nafasi kwa Vishoka kutumia muda huo kulaghai Wananchi" ameeleza ndugu Mgeni
Kwa upande wake Meneja wa DAWASA Kibamba, Mhandisi Barnabas Taligunga ameeleza kuwa Mamlaka imeshajipanga kutatua changamoto ya huduma ya maji Makurunge kupitia mpango wa muda mfupi na muda mrefu ambapo mpango wa muda mfupi unaenda kukamilika Mwezi Machi 2026.
"Kwa upande wa Makurunge tunaenda kutatua changamoto ya maji kupitia mpango wa muda mfupi wa kuongeza msukumo wa maji katika eneo hili, tukishaongeza msukumo wa maji tutasogeza huduma ya maji katika mashina yote ambayo hayana huduma ya maji na kuungia wananchi huduma ya maji, kazi ambayo itakamilika mapema Mwezi Machi 2026." ameeleza Mhandisi Taligunga
Taligunga ameongeza kuwa mpango wa muda mrefu ni ukamilishaji wa usanifu wa mradi mkubwa wa maji ambao utatekelezwa katika mwaka wa fedha 2026/2027 na kuwashukuru Wananchi wa Makurunge kwa kutoa eneo la ujenzi wa tenki.
