DAWASA YAWASHUKIA WATEJA MAJUMBANI WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA

Katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja Watumishi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) wameendelea na zoezi la kutoa huduma bora na kwa ufanisi kwa wateja kwa kuwasogezea huduma kwenye makazi sambamba na kauli mbiu ya mwaka huu isemayo
Ni zaidi ya Matarajio
Hayo yamebainishwa na Meneja wa DAWASA Kinyerezi Ndugu Crossman Mkere wakati wa mahojiano maalum na kipindi cha Radio Tumaini kilicholenga kuelezea DAWASA na wiki ya Huduma kwa Wateja.
Ameleeza kuwa tangu mwanzo mwa wiki hii, DAWASA katika Mikoa yake 23 ya Kihuduma imekuwa ikipita mitaani kusikiliza na kutatua changamoto za wateja wake kwa kusogeza huduma karibu ili kuwafikia wananchi wengi zaidi. Zoezi hili limetekelezwa kwa kuweka madawati maalum katika ofisi za Serikali za mitaa ya kusikiliza wateja.
"Tunaweza kusema kuwa wateja ambao tumewafikia hadi sasa temeweza kufikia matarajio yao na kuzidi, hii inaonesha ni kwa kiasi gani tunaendana na kauli mbiu ya Wiki hii, naomba niwatoe hofu wananchi ambao hawajafikiwa kuwa tutawafikia ifikapo ukingoni mwa wiki hii kwa kuwa zoezi letu ni endelevu," amesema Ndugu Makere.
Akijibu swali la msikilizaji wa kipindi, Ndugu Makere ameeleza kuwa DAWASA inaendelea na jitihada za kuhakikisha inaboresha huduma katika eneo lake la Kihuduma kupitia utekelezaji wa Mradi wa maji Bangulo utakaoenda kujibu changamoto za upatikanaji wa huduma katika eneo la Dar es Salaam ya Kusini.
Mradi unatarajiwa kukamilika Disemba 2024 ambapo utanufaisha wakazi 450,000 wa majimbo matano ya uchaguzi ikiwemo Ukonga, Segerea, Ubungo, Kibamba na Ilala.
Akijibu swali la Msikilizaji mwingine kuhusu ubora na ufanisi wa mita za maji, Meneja wa Ankara Ndugu Asimwe Lukiko amesema DAWASA inashughulikia changamoto za bili za wateja, na pia Mamlaka huzingatia viwango na ubora kwani mita za maji kabla ya kufungwa kwa mteja huthibitishwa na Shirika la viwango (TBS) na Wakala wa Vipimo hivyo kuzifanya kuwa na ubora. "Hivyo kama utapata changamoto yoyote kwenye mita yako ni vyema kutoa taarifa kwa DAWASA kwa msaada zaidi," ameelekeza Ndugu Asimwe.
"Nipende kuwatoa hofu wateja wetu ya kuwa DAWASA tunafuata taratibu zote kuanzia kwenye usomaji wa mita hadi uandaaji wa bili ya mteja, kabla ya kutuma bili ya mteja kulingana na matumizi yake, mteja hutumiwa ujumbe wa kuhakiki usomaji wa mita yake, hii ni katika kumfahamisha mteja zoezi zima kabla hajapata bili na endapo unachangamoto karibu kutoa taarifa kwetu kupitia mawasiliano yetu rasmi ya 0800110064 na sisi tutakuhudumia," amesema Ndugu Lukiko.
Pia, Ndugu Lukiko ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wananchi kutoa ushirikiano wakati za zoezi la usomaji mita linalofanyika kila tarehe 10 -15 ya kila mwezi ili kuepusha sintofahamu na changamoto za bili.