Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAWATEMBELEA WATEJA WAKUBWA, YASISITIZA ULIPAJI BILI
28 Aug, 2025
DAWASA YAWATEMBELEA WATEJA WAKUBWA, YASISITIZA ULIPAJI BILI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imetembelea wateja wakubwa kupitia mashirika binafsi na Taasisi za Serikali kwa lengo la kuboresha huduma, kubaini changamoto zao pamoja na kuhimizia ulipaji wa bili za maji kwa wakati.

Wateja waliotembelea ni pamoja Shirika la Nyumba ya Taifa (NHC), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mashirika Binafsi ni Ubungo Plaza, Kiwanda cha Bomba za Chuma (TSP), Ubungo Business Centre pamoja na Kiwanda cha NIDA Textile.

Afisa Biashara wa DAWASA Magomeni, Bi. Ruth Museru amesema Mamlaka inaendelea na zoezi maalum ya kupitia nyumba kwa nyumba na pia kuwatembelea wateja wakubwa ili kutoa elimu na kufuatilia wateja wenye madeni ya huduma.

"DAWASA Magomeni tunaendelea na zoezi la kuwatembelea wateja wakubwa ambao ni TBS, Shirika la Nyumba la Taifa, Chuo cha Usafirishaji NIT pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu huduma, kuwahamasisha ulipaji wa bili za maji kwa wakati pamoja na kupokea changamoto za huduma," ameeleza.

Aidha, Bi. Museru ametoa rai kuwa lengo la Mamlaka ni kutoa huduma bora inayokidhi matarajio ya wateja na kuhakikisha huduma ilipwe kwa wakati.

"Mara kwa mara tunaendelea kuwakumbusha wateja juu ya ulipaji wa bili za maji kwa wakati ili kupunguza malimbikizo ya madeni ambayo yanaweza kuathiri upatikanaji wa huduma ya maji endapo hayatolipwa kwa wakati na tumefurahi kuona wateja wanaridhika na huduma zetu na kuahidi kuongeza ushirikiano ili kuboresha zaidi," amesema.

Kwa upande wake, Johnson Lema ambaye ni Afisa Fedha kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), ikiwa ni sehemu ya Taasisi za Serikali zilizotembelewa ameipongeza DAWASA na kutoa wito kuzidi kuboresha zaidi huduma kwa wateja kwa kuongeza wigo kwa wateja kutoa mrejesho wa huduma kwa Mamlaka ili panapohitajika maboresho ya kihuduma yafanyike.

"Nimefurahi DAWASA kutufikia taasisi yetu leo, ni jitihada kubwa lakini bado kuna haja ya kutoa elimu zaidi juu ya ulipaji wa bili za maji ili kuisaidia Mamlaka kuweza kuboresha huduma zake," amesema.