DAWASA YAWATENGEA SAA 72 WAKAZI TEGETA A

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar Es Salaam (DAWASA), Mkoa wa Kihuduma Mivumoni imetenga siku tatu za kuwasikiliza wananchi juu ya kero na kuzitafutia ufumbuzi kupitia dawati maalumu ya huduma kwa wateja.
Dawati hilo limeanza Julai 24 hadi 26, 2025 ambapo wateja wa mtaa wa Tegeta A Kata ya Goba Wilaya ya Ubungo wamefika kupata huduma mbalimbali ikiwemo kutoa ushauri na mapendekezo kwa DAWASA ya namna ya kuboresha huduma za maji.
Afisa Biashara wa DAWASA Mivumoni, Shedrack Mbwambo ameelezea umuhimu wa uwepo wa dawati hilo la huduma kwa wateja kwa siku tatu (sawa na saa 72) na muitikio waliokuwa nao wananchi wa eneo hilo.
Amesema lengo kubwa la ufunguzi wa dawati hili la huduma kwa wateja ni kuwasogezea wananchi huduma karibu.
“Hapa wanaweza kupata huduma ya kuunganishiwa majisafi, kuzungumza na wateja wenye madeni ya muda mrefu, lakini pia kupokea na kusikiliza maoni ya wananchi juu ya huduma za Mamlaka kwa lengo la kuboresha zaidi," amesema Mbwambo.
Mbwambo amesema muitikio wa wananchi kwa siku ya kwanza umekuwa mkubwa na kuwaomba wananchi waendelee kujitokeza katika madawati ya huduma kwa wateja pindi yanapofunguliwa kwani ni njia rahisi ya kukutana na kuwasikiliza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Tegeta A, Protas Luanda ameridhishwa na ufunguzi wa dawati la huduma kwa wateja akisema hatua hii ni mwanzo wa kuboresha huduma na ushirikiano kati ya wananchi na DAWASA huku akipongeza hatua hii ya Mamlaka kutoka na kuwafata wananchi kuwasikiliza.
Maria Moshi, mkazi wa mtaa wa Tegeta A, amesema kitendo cha kuwafuata wananchi na kuwasikiliza kitaongeza ukaribu kati yao na DAWASA huku akiomba utaratibu huu uwe wa mara kwa mara kuhakikisha huduma bora kwa kila mwananchi.
"Leo tumeweza kufika kwa wingi hapa ni kwa kuwa DAWASA wameshuka chini kutusikiliza huku mitaani, tunafuraha kwakuwa changamoto nyingi tulizokuja nazo hapa zimesikilizwa na kupatiwa ufumbuzi," amesema.