MHANDISI MWAJUMA WAZIRI ATEMBELEA MITAMBO YA RUVU, ASISITIZA KASI YA USAMBAZAJI MAJI
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri ametembelea mitambo ya kuzalisha maji ya Ruvu Juu na Chini Mkoani Pwani na kusisitiza DAWASA kusimamia kikamilifu kasi katika usambazaji Maji ili yawafikie Wananchi wote.
Katika ziara hiyo, Mhandisi Waziri ameambatana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mhandisi Mkama Bwire pamoja na Menejimenti ya DAWASA
Baada ya kujionea uzalishaji unavyoendelea vizuri kukiwa na maji ya kutosha, Mhandisi Waziri ameitaka DAWASA kuhakikisha maji yanayozalishwa yanasambazwa kwa kasi ili yawafikie wananchi.
Mhandisi Waziri amesema Serikali ya awamu ya Sita, chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Maji katika Mikoa ya Dar na Pwani na imedhamiria kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma ya maji bila kuwa na changamoto yoyote na ikiwa karibu na makazi yao na wao kama wasaidizi wake, wanapaswa kutekeleza hilo kwa vitendo.
