WAKAZI KIMARA BARUTI, MBEZI BEACH HADI MSIGANI KUANZA KUNUFAIKA NA HUDUMA YA MAJISAFI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inaendelea na zoezi la maunganisho ya huduma ya maji kwa wakazi wa maeneo mbalimbali ya Kata za Mbezi na Kimara ili kuhakikisha lengo la Serikali la kufikisha huduma ya majisafi kwa wananchi likitekelezwa kupitia Mkoa wa Kihuduma wa DAWASA Ubungo.
Kupitia zoezi hilo, wateja wapya zaidi ya 30 kutoka Mitaa ya Msakuzi, Mbezi, Makabe, Msumi, Msigani wa kata ya Mbezi na mtaa wa Baruti uliopo kata ya Kimara wamepatiwa vifaa vya maunganisho mapya.
Sambamba na ugawaji wa vifaa hivyo, elimu mbalimbali za utunzaji bora wa miundombinu ya maji, umuhimu wa ulipaji bili kwa wakati zilitolewa pamoja na kuwashirikisha kwenye mikakati ya kuzuia upotevu wa maji.
Aidha wateja walikumbushwa juu ya umuhimu wa kuwa na mawasiliano ya karibu na Mamlaka kwa lengo la kupata ufafanuzi au kutoa taarifa mbalimbali zinazohusu huduma kupitia namba 0735 451 865 (DAWASA Ubungo) au namba 181 (Kituo cha huduma kwa wateja, bila malipo).
