Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAWEKEZA MILIONI 200 WAKAZI PUGU STESHENI
16 Jan, 2026
DAWASA YAWEKEZA MILIONI 200 WAKAZI PUGU STESHENI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imekabidhi mabomba kwa ajili ya utekelezaji mradi wa huduma ya majisafi katika eneo la Kibiriko, Mtaa wa Pugu Stesheni, Kata ya Pugu Stesheni, Wilaya ya Ilala ambao utanufaisha wakazi takriban 8,300 katika eneo hilo.

Makabidhiano hayo yamefanyika baina ya DAWASA na Uongozi wa Serikali ya Mtaa na Kata ya Pugu Stesheni kwa lengo la kusogeza na kuimarisha huduma ya maji katika eneo hilo ukihusisha mabomba yenye umbali wa kilomita 11.7 yenye kipenyo cha inchi 6,4, 3, 2 na inchi 1.5.

Akizungumza katika tukio hilo, Meneja wa DAWASA Mkoa wa Kihuduma Ukonga, Mhandisi Honest Makoi amesema mradi huo wenye thamani ya Shilingi Milioni 226 unatekelezwa kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi 2026 na utaondoa changamoto ya upatikanaji maji iliyopo katika eneo hilo la Mtaa wa Kibiriko.

"Tupo hapa kukabidhi vifaa kwa ajili ya  utekelezaji wa mradi wa Majj Kibiriko utakaokuwa na mtandao wa mabomba kwa urefu wa kilometa 11.75 na uliosanifiwa kwa matumizi ya miaka 20 kuhudumia wananchi 8,340 katika kaya 150. Utekelezaji wa mradi huu unaanza wiki hii na utakuwa wa miezi mitatu hivyo tunatoa rai kwa wananchi kutoa ushirikiano, kulinda na kutunza miundombinu hii kipindi chote cha utekelezaji wa mradi," amesema Mhandisi Makoi.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Pugu Stesheni, Mheshimiwa Salumu Shaibu Omari ameishukuru Serikali kupitia DAWASA kwa kuleta mradi huu kwani wananchi wa eneo hili la Kibiriko wamekuwa wakipata changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa muda mrefu.

"Wananchi hawa wa Kibiriko wamekuwa wakihangaika na shida ya maji hadi kufikia kununua kwa gharama kubwa ya ndoo moja kwa shilingi elfu moja, lakini kwa ushirikiano na ujio wa mradi huu changamoto ya maji inakwenda kutoweka katika Mtaa huu," amesema Mheshimiwa Omari.

Baada ya kupokea mabomba hayo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Pugu Stesheni, Shukuru Mohammed Mwinjuma amewataka wananchi wa Kibiriko kuheshimu, kuilinda na kuitunza miundombinu ya maji kwani kwa kufanya hivyo wanalinda rasilimali yao muhimu na kupata huduma endelevu ya majisafi na salama.

Mradi wa kuongeza mtandao wa maji katika eneo la Kibiriko, Mtaa Pugu Stesheni ni matokeo ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa usambazaji maji Dar es Salaam ya Kusini (Bangulo) uliotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliokamilika mapema Aprili 2025.