DAWASA YAZIDI KUCHAGIZA MALENGO YA SERIKALI HUDUMA ZA MAJI

Katika hatua ya kufanikisha adhma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya majisafi kikamilifu, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)kupitia Mkoa wa kihuduma Mapinga imefanikisha zoezi la utoaji wa vifaa vya maunganisho mapya ya maji kwa wateja 120.
Wananchi wa maeneo ya Kiharaka, Kibosha, Vikawe, Kerege, Kiembeni, Udindivu, Mingoi, Mpiji na Changuhela wamepatiwa vifaa na kufungiwa huduma.
Zoezi hilo limesimamiwa na Mhandisi Hamad Omary, ambapo lilienda sambamba na utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya mifumo sahihi ya malipo ya huduma, ulinzi wa miundombinu ya maji pamoja na Mawasiliano rasmi ya Mamlaka kwa Wateja.
Mbali na hapo, Mhandisi Omary aliwakumbusha wananchi kutumia ofisi za DAWASA kupata ufumbuzi wa changamoto zao na kutumia namba ya huduma kwa wateja Mapinga ambayo ni 0734 451863 kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa changamoto za kihuduma.