DAWASA ZINGATIENI MAONI YA WANANCHI KUBORESHA HUDUMA ZA MAJI - MHE KUNENGE

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge ametoa wito kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar Es Salaam (DAWASA) kufanya kufanya tathmini ya utendaji kazi wake kupitia maoni ya Wananchi ili waweze kujiimarisha katika kuboresha huduma za Maji
Mheshimiwa Kunenge ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha watumishi wa DAWASA cha kufunga na kufungua mwaka wa fedha 2025-2026 kilichofanyika Mkoani Pwani.
Ameeleza kuwa ni muhimu kwa DAWASA Kufanya tathmini yake ya utendaji kwa kuzingatia hali halisi iliyopo kwa wananchi juu ya upatikanaji wa huduma za Majisafi na Usafi wa Mazingira na hapo watakua wamejipima vyema.
"Ni muhimu DAWASA mnapofanya tathmini ya utendaji kazi kwa mwaka wa fedha ulioisha na kuainisha mipango kuelekea Mwaka mpya wa fedha 2025/2026 kuzingatia maoni kutoka kwa Wadau muhimu ikiwemo Wananchi, Viongozi wa Chama na Serikali ambao huwakilisha wananchi lakini zaidi kushuka kwa wananchi na kuchukua maoni yao katika maeneo husika ili kupata uhalisia wa hali ya huduma za Maji" ameeleza Mheshimiwa Kunenge
Aidha Mhe. Kunenge amewaasa watumishi wa DAWASA kufanya kazi kwa juhudi na umoja kama timu ili waweze kuwapatia wananchi huduma bora na thamani ya fedha iliyowekezwa na Serikali ionekane na kuleta tija.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe. Nickson Simon amewapongeza DAWASA kwa hatua ya kufanya tathmini ya utendaji kama taasisi na kuwaasa kuwa ili kupata mafanikio ni muhimu tathmini hii ikafanywa pia na mtumishi mmoja mmoja kwani itakua chachu ya maendeleo katika utoaji huduma ya majisafi.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Mkama Bwire amemshukuru kwa ushirikiano mkubwa uliopo kati ya DAWASA na Serikali ya Mkoa wa Pwani ambayo huwarahisishia utendaji kazi na kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma kwa wakati.
"Katika Mkoa wa Pwani ndani ya kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan zimetolewa fedha zaidi ya bilioni 220 kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za Maji kupitia utekelezaji wa Miradi mbalimbali" ameeleza Mhandisi Bwire.
Bwire amesema kuwa ni jukumu la Mamlaka kuhakikisha uwekezaji huu mkubwa katika Mkoa wa Pwani unaleta tija kwa watumishi kufanya kazi kwa juhudi na kuwafikishia wananchi huduma ya majisafi.