Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
DC MPOGOLO AFUNGA VIKAO KAZI DAWASA NA VIONGOZI WA MITAA MKOA WA DAR ES SALAAM
02 Mar, 2025
DC MPOGOLO AFUNGA VIKAO KAZI DAWASA NA VIONGOZI WA MITAA MKOA WA DAR ES SALAAM

Ahimiza kushikamana ili kutatua changamoto za maji kwa wananchi

Mkuu Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo ameipongeza Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kukutana na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wa Wilaya ya Ilala kwa lengo la kuwashirikisha wananchi wanapata huduma ya maji na majibu ya changamoto zao kwa wakati.

Akizungumza wakati wa kufunga kikao kazi cha Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Mpogolo amesema DAWASA imekuwa mfano bora wa kiutendaji kwa kuwaita pamoja jumla ya Watendaji 159 waliopo katika mitaa yote ya Wilaya ya Ilala na kutoa elimu kuhusu masuala ya maji kwa jamii.

"Nawapongeza sana DAWASA kwa wazo la hatua za kuwashirikisha Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kwa kuwatembeza katika vyanzo na miradi ya maji pamoja na kuwapatia elimu juu ya utunzaji wa miundombinu ya maji na Utoaji taarifa mbalimbali zikiwemo upotevu wa maji na uharibifu wa miundombinu ya maji." Amesema Mhe. Mpogolo.

"DAWASA imefanya jambo kubwa sana ambalo hakuna Taasisi yoyote iliyowahi kuwaita Wenyeviti wote wa Serikali za Mitaa na kuwapatia fursa hii ambayo itasaidia sana kupunguza malalamiko kwa wananchi kwa kuwa tayari wameelimika hivyo iwe ni chachu ya kupata majibu yanayohusu changamoto za maji kwa wananchi tunaowaongoza hivyo tushikamane ili kuwahudumia vizuri wananchi." Amesisitiza Mhe. Mpogolo.

Aidha, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire amewashukuru Wenyeviti hao kwa kushiriki katika Ziara na Kikao kazi hicho na kuamini kuwa maazimio ya zoezi hili litasaidia kuhudumia wananchi wa Mitaa yetu.

"Kupitia ushirikiano huu, DAWASA tunaamini kuwa tunaenda kuwa Mabalozi wazuri na kushirikiana kutekeleza na kutatua changamoto zilizopo katika maeneo yetu zikiwemo upatikanaji wa majisafi na kudhibiti upotevu wa maji". Amesema Mhandisi Bwire.

DAWASA imekamilisha hatua ya kwanza ya kuendesha ziara na vikao kazi kwa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa 582 iliyopo katika Mkoa wa Dar es Salaam iliyolenga kujenga mashirikiano katika kutatua changamoto za maji kwa wananchi katika mitaa hiyo.