Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
VISIMA VYA AKIBA KUTUMIA KUPUNGUZA CHANGAMOTO YA MAJI
08 Dec, 2025
VISIMA VYA AKIBA KUTUMIA KUPUNGUZA CHANGAMOTO YA MAJI

Waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso (Mb) ametoa wito kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na Pwani kuendelea kuwa watulivu, hususan katika kipindi hiki cha ubahaba wa maji, akieleza kuwa ni kipindi cha mpito kilichobeba matumaini

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya upatikanaji wa maji Mkoa wa Dar es Salaam, Waziri Aweso alisema kuwa malengo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Wizara ya Maji ni kuhakikisha huduma ya maji inafikiwa kwa wananchi wote huku akisisitiza umuhimu wa kila mtumishi wa DAWASA kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano ili changamoto za maji zitatatuliwa haraka.

“Mhe. Rais ametuagiza tuhakikishe tunafanya kila linalowezekana kusaidia Wananchi katika kipindi hiki. Ni vita tunayopigana kuhakikisha kila mtu anapata Maji safi na salama. Tutafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha maji yaliyopo yanawafikia wananchi,” alisema Waziri Aweso.

Katika ziara yake, Waziri Aweso alitembelea maeneo kadhaa ikiwa ni pamoja na Kimara, Magufuli Hosteli Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bunju, Kawe na Mwananyamala na kudhibitisha upatikanaji wa maji katika baadhi ya maeneo huku akibainisha kwamba bado kuna baadhi ya sehemu ambazo huduma bado haijafika kikamilifu.

“Tumepita maeneo mengi, tumeyajionea matanki yamejaa maji, na tumepata taarifa huduma inapatikana sehemu nyingine. Nataka kuwahakikishia wananchi kwamba maeneo yote ambayo hayajafikiwa maji, yatafikiwa na tutahakikisha maji yanayofika yanahifadhiwa ipasavyo,” alisema Waziri Aweso.