HOJA ZA WANANCHI MATOSA ZAPATIWA UFUMBUZI

Wakazi takribani 491 wa maeneo ya Kings, Ruaha na Kwa Msami katika Kata ya Kimara wilayani Ubungo, wanatarajia kupata afueni ya kudumu ya huduma ya maji baada ya kutambulishwa rasmi kwa mradi mdogo wa upanuzi wa mtandao wa maji wa Matosa ulioanza kutekelezwa.
Mradi huo, unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), unalenga kuboresha huduma ya maji kwa kaya takribani 800 maeneo ya Goba, Mbezi na Matosa, hatua inayotarajiwa kumaliza adha ya kusuasua kwa huduma kwa wakazi wa maeneo hayo.
Mamlaka inatekeleza mradi huu kama sehemu ya mkakati wa kuhakikisha kila mkazi wa Dar es Salaam na Pwani anapata huduma ya maji safi na salama ifikapo mwaka 2030, huku wakisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa jamii katika utekelezaji wake.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Mhandisi wa Miradi, Ndugu Shija Mbonje amesema mradi unatekelezwa kwa umbali wa Kilomita 13, ikiwa kilomita 1.5 zitatekelezwa eneo la Kings ili kutatua adha ya msukumo mdogo wa maji na mara nyingine ukosefu wa maji eneo hilo.
“Mradi huu unakwenda kujibu hoja za wananchi za muda mrefu, vilevile Mamlaka imejipanga kukamilisha mradi huo kwa wakati ili kuboresha huduma kwa wakazi hao,” amesema Mhandisi Shija.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kilungule B, Ndugu Henry Dimoso akizungumza katika kikao cha utambulisho wa mradi huo amesema utekelezaji wa mradi huo ni habari njema kwa wananchi wake na unatoa matumaini mapya.
“Tunaupokea mradi huu kwa moyo wa shukrani na matumaini makubwa. Tunajua utaleta afueni kwa wakazi wetu na kupunguza adha ya ukosefu wa maji kwa muda mrefu,” amesema Ndugu Dimoso.