HUDUMA KWA WATEJA IIMARISHWE - Waziri Aweso

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amezitaka taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maji kuimarisha eneo la Utoaji wa Huduma kwa Wateja ili kuimarisha uhusiano na wananchi wanaotumia huduma ya maji.
Waziri Aweso ametoa maelekezo hayo Jijini Dodoma wakati wa Kikao cha Kisekta kuelekea utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Maji 2024/2025.
"Katika eneo la Huduma kwa Wateja bado kuna changamoto tunazopaswa kuzifanyia kazi, unakuta mwananchi anapiga simu kutoa taarifa lakini simu haipokelewi ama ikipokelewa taarifa haifanyiwi kazi kwa wakati," amesisitiza.
Akizungumza katika semina hiyo, Naibu Waziri Wizara ya Maji, Mhe. Andrea Kundo (Mb) amewaelekeza Watumishi wa Sekta ya Maji kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu ili ilete tija inayokusudiwa.
"Tunahitaji kuwa na miradi endelevu, yenye ubora unaostahili. Ni muhimu tukazingatia ubora unaotakiwa kwa kufuata tararibu zote stahili, tufanye kazi kimkakati na kwa weledi," amesisitiza.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri amesisitiza watumishi wote Sekta ya Maji kufanya kazi kwa kushirikiana ikizingatiwa kuwa lengo la taasisi zote chini ya Wizara ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi.
Aidha, amewasisitiza watumishi wote kuhakikisha wanafanyia kazi kwa wakati taarifa za upotevu wa maji.
"Tubadilike, tuboreshe uhusiano na wananchi na viongozi wa maeneo tunayohudumia ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa wa upotevu wa maji na kuzifanyia kazi kwa wakati," amesisitiza.