HUDUMA YA MAJI YAIMARISHWA MBURAHATI NHC, WANANCHI WAPONGEZA

Jumla ya wakazi 600 watanufaika na maboresho makubwa ya huduma ya maji mtaa wa Mburahati NHC, kata ya Mburahati, Wilaya ya Ubungo.
Ni baada ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuanza utekelezaji wa mradi wa maji Mburahati kwa mroso wenye lengo la kuhudumia wakazi wa eneo hilo kutokana na kupata changamoto ya huduma ya maji kwa muda mrefu.
Mradi wa maji Mburahati kwa mroso unaogharimu kiasi cha Shilingi Milioni 5, utahudumia maeneo ya Mburahati NHC, Udzungwa, Tegemeo, Ruaha na Katavi na kuwapatia huduma bora ya majisafi na salama kwa wananchi.
Akizungumza utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi wa Miradi mkoa wa kihuduma Magomeni, Mhandisi Bertha Ambangile amesema mradi huo ambao chanzo chake ni kisima cha maji kwa mroso utasaidia kutoa huduma ya majisafi kwa wakazi wa eneo hilo ambao walipata changamoto ya maji kwa muda mrefu.
"Mradi utaenda kusaidia kupunguza changamoto ya maji kwa wakazi wa Mburahati NHC na maeneo mengine ya jirani, chanzo chake ni kutoka kwenye kisima cha maji cha kwa mroso," amesema Mhandisi Ambangile.
Mhandisi Ambangile amesema kazi inayoendelea kwa sasa ni kusambaza bomba za inchi 2 kwa umbali wa mita 300 na ujenzi wa vizimba vitano (5) vya kuchota maji.
Kisima cha maji kwa Mroso kina uwezo wa kuzalisha maji lita za ujazo 15,840 kwa saa 1 na kufika lita 380,160 kwa saa 24 (siku moja).
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Mburahati NHC, Ndugu Raphael Mteka ameipongeza DAWASA kwa kutekeleza mradi huu ukizingatia wingi wa wakazi katika eneo hili wana uhitaji wa huduma ya maji.
"Naishukuru sana DAWASA kazi kubwa wanayoifanya ili kuhakikisha wananchi wa eneo hili wanapata huduma ya maji, kwa sasa tuna imani baada ya kuona kasi ya utekelezaji wa mradi huu ambao unakwenda kumaliza kabisa changamoto ya maji hapa mtaani," amesema Ndugu Mteka.
Ndugu Sharifa Kipaumbele, mkazi wa mtaa wa Tegemeo ameishukuru DAWASA kwa kusikia kilio chao cha muda mrefu kwa kukosa maji na sasa wana matumaini ya kupata huduma.
"DAWASA mnatusaidia sana kwa hii changamoto ya maji sasa mnaenda kumtua mama ndoo ya maji kichwani," amesema Ndugu Kipaumbele.