Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
KATIBU MKUU WIZARA YA MAJI AIPA TANO DAWASA KUSHIRIKIANA NA WENYEVITI WA MITAA
02 Mar, 2025
KATIBU MKUU WIZARA YA MAJI AIPA TANO DAWASA KUSHIRIKIANA NA WENYEVITI WA MITAA

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kwa ubunifu mkubwa wa kukutana  na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa katika Mkoa wa Dar es salama na kushirikiana nao kwa nia ya kuboresha huduma za Majisafi na Usafi wa Mazingira.

Mhandisi Mwajuma amesema hayo katika kikao kazi cha DAWASA na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa katika Wilaya ya Ilala katika muendelezo wa vikao kazi vinavyolenga kuboresha ushirikiano katika kuhudumia Wananchi katika mitaa 159 ya Wilaya ya Ilala.

"Jukumu la Wizara ya Maji ni kuhakikisha Jamii inapata huduma ya Majisafi na salama na uondoshaji wa Majitaka, kwa kutambua umuhimu wa kundi hili la Wenyeviti kama jeshi kubwa tunaomba mshirikiane vyema na DAWASA katika upatikanaji wa taarifa za uvujaji na nyinginezo zinazohusu Sekta ya maji katika mitaa yetu." amesema Mhandisi Waziri

"Tumeshuhudia baadhi ya Wananchi wakikosa njia sahihi ya kutoa taarifa na wakati mwingine kuwatafuta viongozi wakuu kama Waziri na Katibu wakuu kutoa taarifa, lakini kwa kutumia fursa hii taarifa nyingi zitakuwa zikipatikana kupitia Wenyeviti wa Serikali za Mitaa ili wananchi waweze kupata majibu kupitia ushirikiano huu na kuweza kuwabaini wanaohujumu miundombinu ya Maji." amesisitiza Mhandisi Waziri.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mtendaji DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire amewashukuru Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na kuwaomba ushirikiano katika kuhakikisha Wananchi katika maeneo yao wanapata taarifa sahihi za huduma za Majisafi na Usafi wa mazingira.

"Wenyeviti wa Mitaa ndio wenye Wananchi hivyo kwa ushirikiano huu tutafanikiwa kuwahudumia Wananchi katika suala la upatikanaji na matumizi ya majisafi na salama katika maeneo yetu." Amesema Mhandisi Bwire.

Kikao kazi cha Wenyeviti wa Serikali za Mitaa katika Wilaya ya Ilala kinahitimisha vikao kazi vya Mamlaka na Watendaji hao vilivyofanyika katika Wilaya Tano za Mkoa wa Dar es Salaam na kuwakutanisha Wenyeviti takribani 582 kutoka katika mitaa mbalimbali ya Mkoa.