KAYA 150 ZATAFUTIWA UFUMBUZI UKOSEFU WA MAJI, WENGINE WAITWA

Jumla ya kaya 150 kutoka kata nne za Kibamba, Kiluvya, Kwembe, Msigani na Mbezi Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam wanakwenda kuondokana na changamoto ya upatikanaji huduma ya majisafi majumbani mwao baada ya kupokea vifaa vya maunganisho na kuungwa rasmi na huduma ya majisafi kwa mara ya kwanza.
Akizungumzia wakati wa makabidhiano ya vifaa vya maunganisho mapya ya maji, Meneja Mkoa wa Kihuduma DAWASA Kibamba, Mhandisi Mkashida Kavishe amesema jumla ya kaya 150 zimepatiwa vifaa hivyo na mara moja zoezi la kuwaunga na huduma linaanza huku akisisitiza zoezi hilo ni endelevu mpaka pale kila mwananchi atakapofikiwa na huduma ya maji.
"Kaya hizi 150 tunazozitoa leo ni sehemu ya zoezi endelevu la kuwaungia wananchi huduma ya majisafi, natoa wito kwa wananchi ambao hawana huduma bado kufanya maombi ya huduma ya maji na kulipia huduma hiyo ili tuweze kumuungia maji kwa haraka.
“Na kwa wale ambao wameshatuma maombi waweze kulipia ili kupatiwa huduma," amesema Mhandisi Kavishe.
Kwa upande wake, Ndugu Mwanaisha Ally, Mkazi wa Kata ya Kwembe amepongeza jitihada zinazofanywa na DAWASA kuwaungia wananchi huduma ya maji huku akisisitiza wananchi zaidi kujitokeza na kupata huduma.
"Huduma kwa sasa inaridhisha, unapoomba huduma hii ya maji hukai tena muda mrefu kabla ya kuungiwa maji, sasa maji tuliyoyaona kwa majirani na sisi kwetu tunakwenda kuyatumia rasmi, jambo ambalo litarahisisha kazi nyingi za majumbani kwetu," amesema Ndugu Mwanaisha.
Hatua hii ya kuungia wananchi huduma ya maji ni dhamira ya Mamlaka katika kuongeza idadi ya wateja iliyowaunganishia maji kutoka wateja 32,000 katika mwaka wa fedha 2024-2025 hadi kufikia wateja 72,000 katika mwaka wa fedha 2025-2026.