KILUVYA MADUKANI WAKAMILISHIWA MATENGENEZO, HUDUMA YAREJEA

Wakazi wa eneo la Kiluvya Madukani, Wilaya ya Ubungo wameelezea furaha yao baada ya matengenezo yaliyokuwa yakifanyika na DAWASA katika bomba kubwa na kupelekea eneo lao kukosa maji kwa siku kadhaa kukamilika na huduma kurejea tena.
Hawa Maulid mkazi wa Mtaa wa Makurunge ameeleza kuwa walikosa huduma ya maji kwa takribani wiki mbili baada ya kupokea taarifa kutoka DAWASA kuwa wanafanya maboresho katika bomba kubwa lakini kwasasa yamekamilika na wameanza tena kupata huduma.
"Ni kweli tumepitia changamoto kidogo kwamaana kipindi cha matengenezo hatukua tunapata huduma, kwasasa shughuli zetu zitaendela tena vyema na hata kazi za majumbani zitakua rahisi kwakua huduma ya maji imerejea.
Mhandisi Jackson Richard kutoka DAWASA Kibamba ameeleza kuwa matengenezo yaliyofanyika yalikua yalazima ili kuboresha huduma katika eneo hilo la Kiluvya Madukani na maeneo ya jirani na sasa huduma imeanza kurejea na kuimarika katika baadhi ya mitaa.
"Maeneo baadhi huduma imerejea, hasa eneo hili la Makurunge, ambalo liliathiriwa na matengenezo yaliyokuwa yanaendelea, lakini mitaa hii inapata maji kwa mgao hivyo siku ya Ijumaa hadi Jumapili eneo la Mji Mpya watapata huduma ya maji kama kawaida kulingana na mgao wao kwani matengenezo yamekamilika" ameeleza Mhandisi Jackson.
Kukamilika kwa matengenezo haya katika bomba kuu la Inchi 8 kutanufaisha maeneo ya Madukani, Kiluvya, Makurunge, Tondoroni, Mji Mpya pamoja na Kwa Omari.