Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
KIMARA - BONYOKWA - KINYEREZI WAKAMILISHIWA MRADI WA MAJI
28 Mar, 2025
KIMARA - BONYOKWA - KINYEREZI WAKAMILISHIWA MRADI WA MAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imekamilisha utekelezaji wa mradi wa uboreshaji huduma ya majisafi Kimara - Bonyokwa - Kinyerezi Kata ya Bonyokwa na Kinyerezi.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo Meneja wa Mkoa wa Kihuduma DAWASA Ubungo, Mhandisi Damson Mponjoli amesema kwa sasa mradi umekamilika na hatua iliyopo ni ujenzi wa chemba za kuwekea matoleo pamoja na kuunganisha wateja wapya katika mtandao mpya.

"Mradi wa uboreshaji huduma kwa wakazi kuanzia Kimara - Bonyokwa hadi Kinyerezi umekamilika kwa asilimia mia, na sasa tumeanza kufanya maunganisho ya wateja katika mtandao mpya pamoja na kujenga chemba za matoleo ya maji" amesema mhandisi Mponjoli

Mhandisi Mponjoli ameongezea pia kuwa mradi huu utaenda kunufanisha majimbo matatu ya kiuchaguzi ya Kibamba, Ubungo na Segerea ambayo hali yake ya upatikanaji wa maji ulikuwa sio mzuri kwa kipindi cha nyuma.

"Mradi huu unaenda kuwa suluhu ya changamoto ya maji katika majimbo ya kiuchaguzi ya Kibamba, Ubungo na Segerea ambapo mkandarasi alipatiwa fedha za vifaa na kazi ikaanza kwa haraka na maeneo yote yanayokwenda kunufaika na mradi huu hayatakuwa na shida ya maji tena." amesema Mhandisi Mponjoli.

Kwa upande wa mkazi wa Vinane Bi. Salma Hamadi ameishukuru Serikali na DAWASA kwa kuwakumbuka na kuboresha upatikanaji wa maji katika mtaa wao ambayo ilikuwa changamoto sana.

"Tunaishukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mama yetu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mradi huu ambao unaenda kumaliza tatizo la maji katika mtaa wetu. Pia naipongeza DAWASA na wenyewe wanafanya kazi kubwa kuhakikisha huduma ya maji inaendelea kuimarika sio kwetu tu hata maeneo mengine tunajionea kwenye tv" amesema Bi. Salma

DAWASA inatekeleza mradi wa uboreshaji huduma ya maji Kimara-Bonyokwa-Kinyerezi ambao umehusisha ulazaji wa bomba za inchi 3, 4 na inchi 8 kwa umbali kwa kilomita 9 sambamba na uboreshaji wa miundombinu  ya maji katika eneo la mto jirani na daraja la Bonyokwa Midland.

Mradi huu utanufaisha wakazi wa maeneo ya Kimara Mwisho, Kwa Kindole, Vinane, Kwa Mrema, Kwa Mashaka, Kwa Kichwa na maeneo jirani ya Bonyokwa.