KINONDONI WATENGEWA MUDA KUTATULIWA CHANGAMOTO ZA MAJI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imefungua dawati la huduma kwa wateja katika Ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kwa lengo la kusikiliza, kutatua na kutoa suluhu ya changamoto za wateja juu ya huduma za majisafi.
Afisa Huduma kwa Wateja wa DAWASA Kinondoni, Ndugu Salama Hamidu amesema hatua hiyo inalenga kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi na kutoa majibu kwa changamoto mbalimbali za kihuduma ikiwemo hitilafu kwenye miundombinu, maombi ya maunganisho mapya na nyinginezo zinazohusu huduma ya Maji.
“Kupitia dawati hili, tunapokea kero za wananchi moja kwa moja, tunazifanyia kazi kwa haraka na kuzifuatilia hadi zipate ufumbuzi. Lengo letu ni kuhakikisha changamoto za maji Kibamba zinatatuliwa kwa wakati,” amesema Ndugu Hamidu.
Wananchi wamejitokeza kupata huduma, wamepongeza hatua hiyo, wakieleza imeleta nafuu na kupunguza usumbufu wa kufuata huduma katika ofisi za mbali.
Aweso amesema muitikio wa wananchi kwa siku ya leo umekuwa mkubwa na kuwaomba wananchi waendelee kujitokeza katika dawati la huduma kwa wateja pindi yanapofunguliwa kwani ni njia rahisi ya kukutana na kuwasikiliza.
Mmoja wa wananchi wa Jimbo la Kinondoni, Ndugu Hamida Suleiman amesema uwepo wa DAWASA leo katika Ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni umeongeza matumaini ya kutatuliwa kwa changamoto za muda mrefu za maji.
“Awali tulikuwa tunapata ugumu mkubwa kufuata huduma za DAWASA, lakini leo nimepata urahisi kwa kufikisha malalamiko yangu na kupata majibu hapahapa. Naamini changamoto zetu zitapatiwa ufumbuzi,” amesema Suleiman.
DAWASA inaahidi kuendelea kuboresha huduma zake kwa kushirikiana na viongozi wa serikali na wananchi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa uhakika katika Jimbo la Kinondoni na maeneo jirani.
