KINYEREZI WAHAKIKISHIWA UHAKIKA WA MAJI SAFI NA SALAMA

NI BAADA YA KUKAMILIKA KWA MRADI WA MAJI BANGULO
Imeelezwa kuwa Wakazi wa Kinyerezi wataondokana na adha ya kukosa majisafi inayowakumba sasa baada ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kutangaza kuanza Kusambaza Majisafi katika maeneo yao kuanzia Mwishoni mwa Mwezi Februari 2025.
Hatua hiyo imekuja baada ya kukamilika kwa mradi wa maji wa Bangulo unaogharimu kiasi cha Sh. Bilioni 36.8 ambao utahudumia wakazi zaidi ya 450,000 huku utekelezaji wake ukijumuisha ujenzi wa tenki kubwa la kuhifadhi maji lita Milioni 9 ulioenda sambamba na ulazaji wa mtandao wa bomba wenye Kilomita 108.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Mkama Bwire akiongea na waandishi wa habari waliotembelea maeneo mbalimbali ya kihuduma DAWASA ikiwemo bwawa la Kidunda uliopo Mkoani Morogoro.
"Katika huu mradi wa kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji Dar es salaam ya Kusini ulikamilika kwa asilimia 99, kilichokuwa kimebaki ni kuunganishwa kwa mitambo yetu ya umeme ianze kazi na ndani ya siku mbili hizi tutaanza kuwasha mitambo yetu kwa hatua za majaribio," amesema Mhandisi Mkama.
Bwire amewataka wananchi kwa kipindi hiki kuwa na subira hadi itakapofika ukamilishaji wake tayari kuanza kuyaachia maji hayo.
Kauli ya DAWASA inatoka kipindi ambacho baadhi ya maeneo mathalani ya Kinyerezi yakiwa yanapata huduma ya Maji kwa awamu katika maeneo mengi.
Aidha katika hatua nyingine DAWASA imewaomba wateja wake kuwa na tabia ya kuwa na matenki ya kuhifadhi maji Ili kusudi inapotokea changamoto yoyote waweze kuwa na akiba ya maji.
Bwire ametoa rai hiyo ili wakazi wawe na maji muda wote kwajili ya matumizi yao na wasitetereke pale kunapotokea changamoto, hata hivyo ameeleza Serikali inaendelea na juhudi za kujenga matenki mengine ya maji sehemu mbalimbali.