Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
KISARAWE WAHIMIZWA ULIPAJI WA BILI ZA MAJI KWA WAKATI
24 Jan, 2025
KISARAWE WAHIMIZWA ULIPAJI WA BILI ZA MAJI KWA WAKATI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Mkoa wa Kihuduma wa Kisarawe inaendelea na zoezi la ufuatiliaji wa malipo ya huduma za maji kwa wateja wenye madeni ya bili za maji kwa wateja wa maeneo yote ya kihuduma huku ikiwasisitiza umuhimu wa ulipaji bili kwa wakati.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Biashara wa DAWASA Mkoa wa Kihuduma wa Kisarawe, David Kisoka amesema kuwa watumishi wa Mamlaka kwa sasa wapo mitaaani wanaendelea na kufuatilia madeni nyumba hadi nyumba ili kuhakikisha wateja wanalipa bili na madeni hayo kwa wakati.

"Tunawakumbusha na kuwahimiza wateja wetu wa maeneo yote ya Kisarawe Mjini, Sanze, Umatumbini, Kimani, Chanzige, Bombani, Pugu na kwingineno kulipa bili zao za maji mapema ili kuepuka usumbufu kwani sasa timu za watumishi wa DAWASA zipo katika zoezi maalum la kupita kila nyumba kufuatilia wateja wenye madeni na kuwakumbusha walipe na wale wenye madeni ya malimbikizo kusitishiwa huduma ili yasiendelee kuongezeka", Ameeleza Kisoka.

Ameongeza kuwa zoezi hilo linaenda sambamba na uelimishaji wateja na jamii kwa ujumla kuhusu matumizi sahihi ya maji, utunzaji wa vyanzo vya maji, ulinzi wa miundombinu ya maji, umuhimu wa kulipa bili za maji kwa wakati ili kuwezesha Mamlaka kumudu kutekekeza majukumu ya kutoa huduma toshelevu kwa wateja na kuendeleza miradi maeneo ambayo bado hayajafikiwa.

Mamlaka inasisitiza wananchi na wateja wa DAWASA katika maeneo mbalimbali ya kihuduma kulipa bili zao kwa wakati ili kuepukana na usumbufu wa kusitishiwa huduma pamoja na kuiwezesha Mamlaka utekelezaji wa majukumu muhimu ya kuwapatia wananchi wote huduma ya maji katika maeneo mbalimbali.