KISARAWE YAKUMBUSHWA KUCHANGIA HUDUMA ZA MAJI KWA WAKATI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kupitia Mkoa wa kihuduma DAWASA wa Kisarawe umewakumbusha wateja wa maeneo hayo kulipa ankara zao za mwezi kwa wakati ili kuwezesha Mamlaka kuboresha zaidi huduma zake.
Afisa Biashara wa DAWASA Kisarawe, Ndugu David James Kisoka amesema kuwa kwa mujibu wa mkataba wa huduma kwa wateja, Mteja ana wajibu wa kulipia ankara yake ya Maji kwa wakati kulingana na matumizi yake ya mwezi husika.
"Sisi DAWASA tuna wajibu wa kuhakikisha mteja wetu anapata huduma ipasavyo na kuhakikisha inaendeleza huduma katika maeneo ambayo bado hajafikiwa na kuboresha zaidi katika maeneo mengine, hivyo ni vyema wateja kukumbuka umuhimu wa kulipia huduma kwa wakati sahihi ili kuwezesha huduma ya maji kuwa endelevu," amesema Ndugu Kisoka.
Ndugu Kisoka ameendelea kueleza kuwa kwa sasa zoezi la ufuatiliaji wa wateja wenye madeni nyumba kwa nyumba linaendelea katika maeneo na vitongoji vyote vya Kisarawe Mjini, Kimani, Sanze, Vigama, Pugu, Kwa Mustafa, Dampo, Talian na Mgeule.
"Tunawasisitiza wateja wote wawe na utamaduni wa kulipa bili zao za maji mara wanapopokea ujumbe wa bili ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza kwa kusitishiwa huduma kutokana na malimbikizo ya bili hizo hivyo nitoe rai kwa wateja wetu kulipia huduma kwa wakati kulingana na matumizi," ameeleza.
Mkoa wa Kihuduma DAWASA-Kisarawe unahudumia wateja takribani 7,285 katika kata 4 za Pugu, Kisarawe, Buyuni na Kazimzumbwi.