KITUNDA RELINI WAIMARISHIWA HUDUMA, 300 KUNUFAIKA
Mafundi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mkoa wa Kihuduma wa Ukonga, wanaendelea na hatua za mwisho za maboresho ya miundombinu ya maji yaliyolenga kudhibiti upotevu wa maji na kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wakazi zaidi ya 300 wa Mtaa wa Relini, Kata ya Kitunda, Wilaya ya Ilala.
Maboresho hayo yamehusisha ubadilishaji wa kiungo cha bomba lenye kipenyo cha inchi 6 kilichopasuka katika eneo la Makamba na kusababisha uvujaji mkubwa wa maji pamoja na kuathiri upatikanaji wa huduma kwa wakazi wa Mtaa wa Relini na maeneo jirani.
Bomba hilo lilipasuka kutokana na kuongezeka kwa msukumo wa maji kufuatia kuimarika kwa usambazaji kutoka Mradi wa Maji wa Bangulo, unaohudumia maeneo mbalimbali, ikiwemo Kata ya Kitunda.
Kwa sasa, kazi imefikia hatua za mwisho baada ya kukamilika kwa ubadilishaji wa kiungo hicho cha bomba. Kinachosubiriwa ni kukauka kwa zege lililowekwa kwa ajili ya kuimarisha bomba na kuzuia athari za mkandamizo wa maji. Kukamilika kwa kazi hiyo kutarejesha huduma na kuimarisha upatikanaji wa maji katika maeneo ya Relini, Makamba, Chama cha Biblia na Kitunda Machimbo.
DAWASA inawakumbusha wakazi na wateja wote kushiriki katika kulinda miundombinu ya maji kwa kutoa taarifa za uvujaji au hitilafu mara wanapozibaini kupitia Kituo cha Huduma kwa Wateja kwa kupiga simu namba 181 (bila malipo) au kutuma ujumbe kupitia WhatsApp 0735 202 121. Ushirikiano wa wananchi utaiwezesha Mamlaka kuchukua hatua kwa wakati na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa huduma bora ya maji.
