Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
KOREA KUSINI YAONESHA NIA KUWEKEZA SEKTA YA MAJI DAR, PWANI
22 Apr, 2026
KOREA KUSINI YAONESHA NIA KUWEKEZA SEKTA YA MAJI DAR, PWANI

Ujumbe kutoka Serikali ya Jamhuri ya Korea Kusini imetembelea miradi ya maji ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kujionea jinsi gani Serikali ya Korea inavyoweza kushirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kutoa huduma ya majisafi kwa wananchi wa Mikoa ya Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani.

Akizungumzia ziara hiyo, Msimamizi Kitengo cha Usimamizi wa Upotevu wa Maji DAWASA, Mhandisi Tyson Mkindi amesema ujumbe huo umekuja DAWASA kwa lengo la ushirikiano wa kuendeleza miradi mbalimbali ya maji sambamba na kuangalia namna ya kusaidia kuzuia upotevu wa maji.

"DAWASA tumepata bahati ya kutembelewa na ujumbe kutoka Serikali ya Korea Kusini, ambao umefika kwa nia ya kuangalia fursa  za kuwekeza katika miradi, mitambo ya maji pamoja kutupatia mbinu mbadala za kuzuia upotevu wa maji," amesema Mhandisi Mkindi.

"Ujumbe huu umeanza kwa umetembelea Mtambo wa Uzalishaji Maji Ruvu Chini pamoja na mataki ya kuhifadhi maji kwa lengo la kujifunza na kupata mwanga wa namna ambavyo Serikali ya Korea Kusini inaweza kushirikiana na Mamlaka kufanya uwekezaji wa kupanua mitambo yetu ya maji itakayosaidia kuongeza utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi," ameongeza Mhandisi Mkindi. 

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkuu kutoka Serikali ya Korea Kusini, Mkurugenzi wa Ulsan International Development Cooperation Center (UIDCC), Chanmin Park amesema Serikali yao imeendelea kuwa na utayari wa kushirikiana na DAWASA kuboresha huduma za maji kwa kuangalia sehemu muhimu za kuboresha huduma hususani katika upanuzi wa mitambo ya uzalishaji maji na uzuiaji wa maji yanayopotea baada ya kuzalishwa.

"Tumefurahi kupita Mtambo wa uzalishaji maji wa Ruvu Chini tumeona jinsi gani DAWASA inazalisha maji kwa kiasi gani na mahitaji yalivyo kwa wananchi kuwa ni mengi" amesema ndugu Park