Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
MABALOZI WA MAJI WACHOTA UJUZI UZALISHAJI NA USAMBAZAJI HUDUMA YA MAJI
30 Mar, 2026
MABALOZI WA MAJI WACHOTA UJUZI UZALISHAJI NA USAMBAZAJI HUDUMA YA MAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imeratibu ziara ya mafunzo kwa wanafunzi wa Shule za Sekondari Kibaha na Saranga kutembelea Mtambo wa uzalishaji Maji Ruvu Chini na Tank la kuhifadhi maji Mshikamano liliopo  kata ya Mbezi Wilayani Ubungo ikiwa na lengo la kuwajengea uelewa juu ya uzalishaji huduma ya maji pamoja na usambazaji hadi kwa mtumiaji wa mwisho.

Akizungumza katika ziara hiyo Ndugu Hashura Kamugisha, Afisa mawasiliano DAWASA amesema kuwa Mamlaka inatambua umuhimu wa kutengeneza  kizazi kijacho kinachotambua na kuthamini umuhimu wa huduma ya maji pamoja na utunzaji wa miundombinu ya maji na hivyo ziara za mafunzo kwa vitendo ni muhimu sana kwa wananfunzi hao. 

"Tumefanya ziara nzuri ya mafunzo kutoka kwa Wananfunzi wa Shule za Saranga na Kibaha ambazo ni baadhi ya shule zenye klabu za  Mazingira zinazosimamiwa na DAWASA, kupitia mafunzo haya wamepata nafasi ya kutembelea na kujifunza juu ya shughuli zinazofanywa na DAWASA katika uzalishaji na usambazaji wa mqaji pamoja na jitihada zinazofanywa katika kulinda vyanzo vyetu vya maji na kuthibiti upotevu wa maji katika jamii. 

Kamugisha ameongeza kuwa wanafunzi hawa kupitia ziara hizi za mafunzo wamejifunza thamani halisi ya maji jambo ambalo litasaidia katika mapambano dhidi ya upotevu wa maji, kwa wanafunzi hawa kuwa mabalozi wa kwanza kutoa taarifa pindi wanaposhuhudia upotevu wa maji.

Kupitia mafunzo haya pia Wanafunzi walipata nafasi ya kushiriki zoezi la upandaji miti katika eneo la Mtambo wa  Maji Ruvu Chini unaohudumia Wakazi wa Dar es salaam na Pwani kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi kutunza na kusimamia uhifadhi wa mazingira.

Mwalimu mlezi wa klabu ya mazingira kutoka shule ya sekondari Kibaha, ndugu Evance Makasi ameishukuru Mamlaka kwa kutoa nafasi kwa wanafunzi kujifunza na kujionea hatua mbalimbali za uzalishaji maji kabla hayajafika kwa wateja na  imekuwa chachu kwa wanafunzi kutamani  kuwa wataalamu wa maswala mbalimbali yanayohusiana na maji na usafi wa mazingira,na kuwa mabalozi wema katika kushiriki kupunguza upotevu wa maji katika maeneo wanayoishi. 

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) ni mlezi wa klabu za Mazingira 12 zilizopo katika shule za Sekondari na Msingi Mkoani Dar es salaam na Mkoa wa Pwani.