MADIWANI KIBAHA WAISIFU DAWASA UWEKEZAJI MIRADI YA USAFI WA MAZINGIRA

Baraza la Madiwani pamoja na Wakuu wa Idara wa Halmashauri ya Mji Kibaha wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Mhe.Mussa Ndomba wameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa uwekezaji mkubwa uliofanywa katika mradi wa ujenzi wa mitambo ya kisasa ya kuchakata takatope.
Mhe. Ndomba ameyasema hayo wakati wa ziara ya Madiwani pamoja na Wakuu wa Idara kutembelea mtambo wa kisasa wa kuchakata takatope Mburahati pamoja na utekelezaji wa ujenzi wa mtambo wa Gezaulole, Kigamboni.
"Lengo kuu la ziara hii ni kushuhudia uendeshaji wa mitambo hii na kuona jinsi inavyoweza kuwa katikati ya makazi ya watu pasipo kuathiri jamii inayoizunguka. Hatua hii ni muhimu kabla ya utekelezaji wa ujenzi wa mtambo huu unaotegemewa kujengwa katika Halmashauri ya Mji Kibaha."amesema
Mhe.Ndomba amesema kupitia ziara hiyo wamejiridhisha kwamba mradi huo una manufaa kutekelezwa katika eneo la Kibaha kwani utasaidia kuimarisha huduma ya Usafi wa Mazingira.
Mhandisi Amon Gracephord kutoka Idara ya Miradi na Uwekezaji amesema kuwa DAWASA imewaalika Madiwani pamoja na Wakuu wa Vitengo ili kuwaongezea uelewa jinsi mitambo hiyo inavyofanya kazi na kuonyesha ni namna gani haina athari kwa jamii inayoizunguka.
"Tumepanga kutekeleza mradi wa ujenzi wa mtambo wa kisasa katika eneo la Mitamba, Kibaha utakaokuwa na uwezo wa kuchakata Lita 170,000 kwa siku. Hii itasaidia kuboresha huduma ya Usafi wa Mazingira katika mkoa wa Dar es Salaam na Pwani."ameeleza
DAWASA inatekeleza ujenzi wa mitambo 8 ya kisasa ya kuchakata takatope katika Wilaya 5 za mkoa wa Dar es Salaam ambao unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia.