MAMIA WACHANGAMKIA HUDUMA YA MAJISAFI BANGULO

Ni baada ya kukamilika kwa mradi wa Maji wa Bilioni 36.7
Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imepokea maombi ya maunganisho mapya ya huduma ya maji kwa wakazi zaidi ya elfu nne wa maeneo ya Bangulo, Kata ya Pugu Stesheni Wilayani Ilala waliojitokeza kuomba huduma ya Majisafi baada ya kukamilika kwa mradi wa Usambazaji maji Dar es Salaam ya Kusini maarufu kama Bangulo.
Akizungumza wakati wa zoezi usajili na utoaji elimu kwa waombaji wa huduma hiyo, Afisa Huduma kwa Wateja Mkoa wa Kihuduma DAWASA Ndugu Boniface Mwaibabile amesema kwamba hamu ya muda mrefu kwa wakazi wa Bangulo kinakwenda kuisha kwani sasa wanaenda kunufaika kwa kupata huduma ya majisafi na kwa gharama nafuu.
"Muitikio wa kuomba huduma ya Maji kwa wakazi wa Bangulo ni kubwa , sisi kama Mamlaka tunawahakikishia kwamba watapata huduma ya maji hivi karibuni, tunaendelea na zoezi la kupokea maombi ya maunganisho ya maji kwa kuwa tuna uhakika kuwa huduma itapatikana kwa wakazi wote wa Bangulo na maeneo mengine nufaika", amesema Mwaibabile.
"Zoezi la uandishaji maunganisho ya wateja wapya limeanza sambamba na utoaji wa elimu ya huduma zitolewazo na Mamlaka, hivyo wajitokeze kujaza fomu ili wafanyiwe upimaji wa kutambua mahitaji ili taratibu za maunganisho ya huduma zikamilishwe" Ameongeza Mwaibabile.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Bangulo ndugu Goodluck Mwele mesema kwamba kukamilika kwa mradi huu kumeondoa tatizo kubwa sana kwa wakazi wa Bangulo ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiteseka kwa kukosa huduma ya majisafi.
"Tunaishukuru sana Serikali yetu kwa kupitia DAWASA kukamilisha mradi huu ambao ni mkombozi wa upatikanaji wa huduma ya maji katika Mtaa wetu wa Bangulo, kwa pamoja tupo tayari kulinda miundombinu ya maji na tutachukua hatua kwa waharibu" amesema Mwele.
Naye mkazi wa eneo la Hali ya hewa, Mtaa wa Bangulo bi. Jaqueline Mtei ameiomba Mamlaka kufanikisha kwa haraka zoezi la maunganisho ya maji kwa kuwa wana kiu sana na maji hayo ambayo ni bei nafuu kuliko wanayotumia sasa.
Zoezi la uandikishaji wateja wapya na uelimishaji wananchi kuhusu huduma za maji katika Mtaa wa Bangulo unaendelea katika maeneo ya Bangulo Hali ya Hewa, Serikali ya Mtaa Bangulo na Mwembekiboko.