Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
MATENGENEZO BOMBA MPIJI, KAZI INAENDELEA USIKU NA MCHANA
05 Nov, 2026
MATENGENEZO BOMBA MPIJI, KAZI INAENDELEA USIKU NA MCHANA

Kazi ya matengenezo ya bomba kubwa lenye kipenyo cha inchi 72 katika eneo la Mto Mpiji Wilaya ya Kinondoni iliyopelekea kupungua kwa huduma ya Maji kwa Wakazi wa Bagamoyo hadi Ilala wanaohudumiwa kupitia mtambo wa Ruvu Chini inaendelea.

Kazi hiyo inayofanywa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inategemea kufanyika kwa Saa 96 kuanzia Novermba 3,2026 hadi Novemba 6,2026 huku uzalishaji ukitajwa kuwa chini ya asilimia 60.

Akizungumzia maendeleo ya kazi hiyo, Mhandisi Valentine Njau ameeleza kazi kubwa inayoendelea kwasasa ni kuunganisha bomba jipya na bomba la zamani mara baada ya kazi kubwa ya kulikata kukamilika .

"Mara baada ya Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Albert Chalamila kukagua maandalizi ya kazi hii na kuruhusu utekelezaji wake, DAWASA mara moja tulianza na kazi hii inakwenda vizuri ambapo kwasasa tunaweka viungio katika bomba tulilolikata ili kuunganisha  bomba jipya na la zamani. Ni matumaini yetu tutamaliza ndani ya muda" ameeleza Mhandisi Njau.

Mhandisi Njau ameeleza kuwa kazi hii ilikua ni muhimu kufanyika ili kulinda miundombinu hiyo ya maji na athari zinazoweza kuletwa na mvua za El-Nino zinazotarajiwa jambo ambalo lingeleta adha kubwa kwa wananchi kukosa huduma ya maji.