MATENGENEZO MPIJI YAMEKAMILIKA, KAZI YA USAMBAZAJI MAJI INAENDELEA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imekamilisha kazi ya matengenezo kinga ya bomba kubwa la maji la inchi 72 katika eneo la Mpiji, kata ya Mabwepande hatua inayotajwa kurejea kwa huduma ya maji kwa wananchi walioathirika na upungufu wa huduma kutokana na matengenezo hayo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi DAWASA, Mhandisi Romanus Mwang'ingo amesema matengenezo hayo yamefanyika kwa lengo la kuchukua tahadhari ya kulinda miundombinu dhidi ya athari za mvua ya El nino, hali iliyopelekea kupungua kwa uzalishaji kutoka mtambo wa Ruvu Chini ili kuruhusu matengenezo hayo.
"Tayari tumekamilisha kazi na tumeruhusu maji kuingia katika mabomba makuu ya uzalishaji na matanki ya kuhifadhi Maji, tumeruhusu huduma katika tenki la Chuo kikuu Ardhi pamoja na matenki ya njiani ili kuruhusu kazi ya usambazaji maji kuendelea. Timu za mafundi ziko tayari mtaani kwa ufuatiliaji ili kuhakikisha huduma inaendelea kuimarika"amesema Mhandisi Mwang'ingo
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kihonzile, ndugu Hassani Mnondwe ameshukuru DAWASA kwa kutekeleza kazi hiyo ndani ya muda uliopangwa ambapo pia amewatoa hofu Wananchi kuwa huduma ya Maji itaimarika kwa kuwa DAWASA iko kazini.
"Nitoe rai kwa wananchi kuendelea kuwa watulivu wakati huduma inaendelea kuimarika, timu ya Mafundi ipo mtaani kuhakikisha huduma inarejea kama ilivyokuwa hapo awali" amesema ndugu Mnondwe
Kukamilika kwa matengenezo hayo ni sehemu ya jitihada za DAWASA katika kuboresha miundombinu ya maji sambamba na kuimarisha upatikanaji wa huduma na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kwa uhakika na endelevu.
