MAUNGANISHO YA WATEJA WAPYA YASHIKA KASI MANZESE, TANDALE HADI SINZA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kupitia Mkoa wa Kihuduma Magomeni imeendelea na zoezi la utoaji wa vifaa vya maunganisho mapya ya huduma ya majisafi kwa wananchi wa maeneo ya Manzese, Tandale hadi Sinza ili waweze kunufaika na jitihada za Serikali za kuhakikisha wamepata huduma ya majisafi.
Akizungumza wakati wa zoezi la ugawaji vifaa vya maunganisho mpya, Mhandisi wa Miradi mkoa wa kihuduma Magomeni, Mhandisi Bertha Ambangile amesema zaidi ya wateja 25 wataanza kunufaika na huduma ya maji mara baada ya kukamilika kwa zoezi la maunganisho.
"Tunaamini wateja 25 waliopokea vifaa vya maunganisho mpya ya maji wataenda kunufaika na huduma hiyo baada ya kuwaunganisha huduma ya majisafi," amesema Mhandisi Ambangile.
Sambamba na zoezi la utoaji wa vifaa hivyo, DAWASA Magomeni imetoa elimu kwa wateja hao wapya kuhusu utunzaji wa miundombinu ya maji, matumizi sahihi ya maji, njia rasmi ya kimawasiliano, malipo ya ankara na huduma nyingine zitolewazo na Mamlaka.
Kwa upande wake, mkazi wa Ubungo NHC, Ndugu Rehema Mwakyambiki ameishukuru DAWASA kwa kufanikisha kuwaunganisha na huduma ya majisafi mara baada ya kupokea vifaa vya maunganisho.
"Naishukuru sana DAWASA kwa hatua hii kubwa kwa kufanikisha kupata vifaa vya maunganisho na sasa tunaenda kuunganishiwa huduma ili tuweze kunufaika na huduma ya majisafi," amesema Ndugu Mwakyambiki.
Zaidi ya wateja wapya 25 wa maeneo ya Manzese, Tandale, Sinza, Magomeni na Kigogo wataanza kunufaika na huduma ya majisafi baada ya kukamilika kwa zoezi la maunganisho.
Mamlaka inawasisitiza wananchi wanaohitaji kuunganishiwa huduma ya majisafi kuwasiliana nasi kupitia kituo cha huduma kwa wateja 181 (Bila malipo) au 0735 451 862 DAWASA Magomeni.