Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
MHANDISI BWIRE AWAFUNDA VIONGOZI KUWAJIBIKA NA CHANGAMOTO ZA WANANCHI
07 May, 2025
MHANDISI BWIRE AWAFUNDA VIONGOZI KUWAJIBIKA NA CHANGAMOTO ZA WANANCHI

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mhandisi Mkama Bwire amewataka viongozi waandamizi wa Mamlaka hiyo kuwajibika kwa Wananchi wanaowahudumia ili kuleta na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kuboresha utoaji wa huduma bora za Majisafi na Usafi wa Mazingira. 

Mhandisi Bwire ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi kwa Viongozi waandamizi wa DAWASA unaofanyika Mkoani Morogoro.

"Viongozi wenzangu tunalo jukumu kubwa la kufanikisha malengo ya Serikali ya kufikia asilimia 95 ya upatikanaji Maji mijini 2025, kwa sasa tumefikia asilimia 93 na kama Mamlaka tunahitaji kujitathimini na kuweka mifumo ya uwajibikaji itakayosaidia kuimarisha na kuondokana na changamoto zilizopo ili kuongeza ufanisi zaidi." Amesema Mhandisi Bwire.

"Mamlaka ina nguvu kazi kubwa inayohitaji kusimamiwa na kuratibiwa vizuri kuanzia ngazi ya watumishi wa chini hadi viongozi wa juu. DAWASA ina Watumishi wenye ari na kazi ya kuwatumikia Wananchi. Lakini wapo wachache wanaokwamisha juhudu hizi, huenda sababu mojawapo ni changamoto ya mifumo ya usimamizi na uratibu wa majukumu.  Hivyo tutumie wakati huu kutathimini zaidi mifumo na miongozo iliyopo ili itusaidie kupata matokeo chanya katika utendaji kazi wetu." Amesema Mhandisi Bwire.

Moja ya washiriki wa kikao kazi , Ndugu Crossman Makere ameushukuru uongozi wa Mamlaka kwa kutoa mafunzo na fursa ya kutathmini changamoto za kiutendaji kama viongozi ili kuleta mafanikio katika kazi.

"Kwa niaba ya Viongozi waandamizi wa DAWASA tunaishukuru Menejimenti kwa nafasi hii ya kujifunza na kutathmini, tunaamini baada ya kikao kazi hiki tunatarajia utekelezaji wa maazimio tuliyokubaliana na kuahidi uadilifu zaidi katika utendaji kazi."  Amesema Ndugu Makere.

Zaidi ya viongozi 50 wanashiriki kikao kazi  hicho kinacholenga kuongeza tija na uwajibikaji zaidi mahala pa kazi.