MILIONI 700 KUTATUA CHANGAMOTO YA MAJITAKA SINZA C
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeanza utekelezaji wa mradi wa uboreshaji Usafi wa Mazingira mtaa wa Sinza C, Kata ya Sinza Wilaya ya Ubungo, wenye lengo la kutatua changamoto ya utiririshaji majitaka kiholela hali inayohatarisha afya za wananchi.
Kukamilika kwa mradi huu kutanufaisha wakazi wa mitaa ya Mahakama ya Mwanzo, Sinza, Shebofu, Nyamuyo, Msafiri, Sembule, Shirika, mtaa wa Mwanza pamoja na Maneti.
Msimamizi wa mradi kutoka DAWASA, Mhandisi Justine Kyando amesema mradi huu unahusisha uchimbaji na ulazaji wa bomba zenye ukubwa wa inchi 10 kwa umbali wa kilomita 1.5 pamoja na bomba la inchi 8 kwa umbali wa kilomita 2.9 na utakapokamilika utaenda kunufaika kaya takribani 250.
"Mradi huu tumeuanza Novemba 2025, na tunatarajia kukamilisha ifikapo Aprili 2026, mradi unagharimu kiasi cha Shilingi Milioni 700 na kukamilika kwake kutamaliza tatizo la kujaa mara kwa mara kwa chemba za majumbani kunakosababishwa na water table kuwa juu," amesema Mhandisi Kyando.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mtaa wa Sinza C, Ndugu Fredrick Kapufu ameishukuru Serikali kupitia DAWASA kwakusikiliza ombi lao la kuwekewa mfumo rasmi wa majitaka katika mtaa wao jambo ambalo wananchi wamelipokea vyema.
"Mradi huu umekuja katika wakati sahihi, wananchi wamehamasika sana kujiunga na mfumo wa uondoshaji majitaka ukizingatia wengi wao wamekuwa wakipata huduma kupitia magari ya watoa huduma binafsi ambayo ni gharama kubwa sana, hii itawaletea unafuu wa maisha pamoja kuboresha Mazingira kwa ujumla," amesema Ndugu Kapufu.
Ndugu Jovin Nassoro, Mkazi wa mtaa wa Sinza C ameasa wananchi wenye tabia ya kutiririsha majitaka kiholela mtaani na kuchafua mazingira kuacha tabia hiyo mara moja na badala yake sasa wawe tayari kujiunga na mfumo rasmi wa majitaka kutoka DAWASA ili kupunguza au kumaliza athari za kiafya na kimazingira zinazosababiahwa na tabia hiyo.
