MISUGUSUGU, VISIGA NA KAWAWA WANUFAIKA NA HUDUMA YA MAJI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeendelea kusogeza huduma ya maji safi karibu na wananchi kwa kuwapatia maunganisho mapya wakazi wa maeneo ya Misugusugu, Visiga, Kawawa na Mtongani, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama.
Zoezi hilo limetekelezwa na DAWASA Mkoa wa Kihuduma wa Mlandizi, ambapo zaidi ya wateja wapya 100 kutoka mitaa ya Kichangani, Matuga, Kilangalanga Madafu na Mbwawa wamekabidhiwa vifaa vya maunganisho ya maji safi ili kuwawezesha kupata huduma hiyo katika makazi yao.
Mbali na kugawa vifaa hivyo, DAWASA pia imetoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza miundombinu ya maji, kulipa bili kwa wakati na kushiriki katika juhudi za kudhibiti upotevu wa maji ili kuhakikisha huduma inaendelea kuwa endelevu.
Wananchi wamehimizwa kuendelea kushirikiana na mamlaka hiyo kwa kutoa taarifa kuhusu changamoto za huduma na kupata ufafanuzi kupitia namba *0734 130 133* (DAWASA Mlandizi) au *181*, namba ya huduma kwa wateja inayopatikana bila malipo.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa DAWASA wa kusogeza huduma za maji kwa wananchi na kuongeza idadi ya kaya zinazopata huduma ya maji safi na salama katika Mkoa wa Pwani na maeneo ya jirani.
