MIUNDOMBINU CHAKAVU YA MAJI YAONDOLEWA DUNDA, KAZI INAENDELEA

Kazi ya maboresho ya miundombinu ya maji inayohusisha ubadilishaji wa mabomba chakavu katika eneo la Dunda, Kata ya Pugu inaendelea kutekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kupitia Mkoa wa Kihuduma Kisarawe kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji katika eneo hilo.
Msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Erasto Mwakilulele amesema kuwa Mamlaka inakusudia kuboresha hali ya upatikanaji kwa wakazi wa eneo la Dunda kwa kuondoa mabomba ya zamani na kuweka mapya ili kutoa uhakika wa upatikanaji wa huduma.
"Eneo la Dunda limekuwa na changamoto ya miundombinu chakavu inayosababisha upungufu na upotevu wa maji hivyo Mamlaka inaendelea na zoezi la kubadili mabomba yenye kipenyo cha inchi 4 na inchi 6 kwa umbali wa kilomita 2 na baada ya kazi hii kukamilika hali ya huduma ya maji itaimarika zaidi na wateja watapata huduma ya uhakika yenye msukumo mzuri wa maji", alisema Mhandisi Mwakilulele.
"Kazi hii ya maboresho inahusisha ubadilishaji wa mabomba ya zamani yaliyokuwa katika Mradi wa Jamii yenye kipenyo cha inchi 4 na inchi 6 kwa umbali wa kilomita mbili na yatawezesha kuondoa changamoto ya upotevu wa maji na kuboresha msukumo wa maji katika maeneo ya Dunda A, Forest Hill, Pugu Bombani, Moravian na baadhi ya maeneo ya Bane", amebainisha Mhandisi Mwakilulele.
Kukamilika kwa kazi hii ya maboresho ya miundombinu ya mabomba kutaimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi zaidi ya 1,200 waliopo katika eneo hilo la Dunda, Kata ya Pugu.