MIUNDOMBINU YA MAJITAKA KARIAKOO KUSAFISHWA SAA 24

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imeweka kambi maalumu ya saa 24 katika eneo la Kariakoo ya kuikarabati miundombinu ya usafirishaji na utiririshaji majitaka ili kuyaweka mazingira kwenye hali ya usafi na salama.
Akizungumzia utekelezaji wa kazi hiyo, Msimaizi wa miundombinu ya majitaka wa DAWASA, Mhandisi Mbaraka Mpala amesema kazi hii ni moja ya kipaumbele cha Mamlaka katika kuboresha usafi wa mazingira eneo la Kariakoo na kufanya biashara zifanyike katika hali shwari na yenye usafi.
"Kazi hii tunaifanya usiku zaidi, kwakuwa mazingira ya eneo hili la kibiashara ni ngumu kusafisha wakati wa mchana ambapo watu ni wengi na msongamano ni mkubwa,” amesema Mhandisi Mpala na kuongeza:
“Tunasafisha miundombinu hii ili tumalize tatizo la kuziba mara kwa mara na kutiririsha majitaka mtaani jambo ambalo linahatarisha afya ya wafanyabiashara na wanunuzi wanaoingia na kutoka hapa hali inayosababishwa zaidi na utupaji wa taka ngumu katika mifumo ya majitaka kama vile nguo, mawe, matairi na plastiki."
Mmoja wa wafanyabiashara katika soko la Kariakoo, Lameck Nganjiro amepongeza utaratibu huu wa DAWASA kusafisha miundombinu hii ya majitaka hususani wakati wa usiku ambapo msongamano na shughuli za kibiashara unakuwa umepungua.
"Kariakoo ni eneo linalopokea watu wengi kwa siku, matumizi ya maji yanayogeuka kuwa majitaka ni makubwa sana, miundombinu hii isipoangaliwa mara kwa mara itatumika isivyo sawa na kusababisha kadhia katika eneo hili majitaka yatakapotiririka mitaani, juhudi hizi za DAWASA ni jambo kubwa na tunawapongeza kwa hatua hii," amesema Lameck.