MRADI WA BANGULO UMETUFUTA MACHOZI

Mradi wa Usambazaji Maji Dar es Salaam ya Kusini (Bangulo) umeleta mageuzi makubwa ya upatikanaji wa huduma hiyo kwa wakazi wa Gulukakwalala na Ulongoni B, Kata ya Gongolamboto wilayani Ilala kwa kuwaondolea adha ya muda mrefu.
Mradi huo uliotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) umeyafanya maeneo mengi ndani ya majimbo ya uchaguzi ya Ukonga, Segerea, Ubungo, Kisarawe na Temeke.
Kupitia mradi wa Bangulo wenye gharama ya Shilingi Bilioni 36.9, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji imebadilika ambapo sasa mafanikio na mabadiliko chanya kwenye maisha ya wananchi yameanza kuonekana.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Gulukakwalala, ndugu Augustino Simba amesema kukamilika kwa mradi huu umechangia kwa kiasi kikubwa kustawi kwa jamii kwani maji yanachangia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kila siku.
"Tunaipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya maji, hakika sisi wananchi wa Gulukakwalala tunaona mabadiliko makubwa ambayo yanasaidia ustawi wa shughuli mbalimbali za jamii," amesema ndugu Simba.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Ulongoni B, ndugu Edisa Mwambeleko ameipongeza DAWASA kwa utekelezaji wa mradi huo kwani sasa huduma ndani ya mtaa wake imekuwa imara ikilinganishwa walipokuwa wakitegemea kisima cha maji kama chanzo chao.
"Hapo awali tulikuwa tukitegemea kisima kama chanzo pekee cha maji kwa ajili yetu, tunaishukuru na kuipongeza DAWASA kwa mradi huu na sasa nitoe rai kwa wananchi kuendelea kuwasilisha maombi ili kuunganishwa rasmi katika mtandao na kuanza kunufaika ma mradi," amesema ndugu Mwambeleko.
Ndugu Fatuma Fikiri, mkazi wa mtaa wa Gulukakwalala amesema mradi wa maji Bangulo sambamba na kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji lakini pia unachangia kupungua kwa uwezekano wa kuibuka kwa magonjwa ya milipuko kama kipindipindu na homa za matumbo.
"Mradi huu umeheshimisha kina mama kwani tulikuwa tukisumbuka kutafuta maji, hivi sasa tunaweza hata kufanya biashara ndogondogo kama uuzaji wa juisi, vyakula, na usafi wa vyombo vya kutokana na upatikanaji wa maji ya uhakika," ameeleza ndugu Fikiri.
Kupitia mradi wa maji Bangulo, DAWASA imeonesha wazi jinsi uwekezaji kwenye huduma muhimu kama maji unavyoweza kubadilisha maisha ya watu. Ulongoni B na Gulukakwalala sasa ni mfano wa mabadiliko yanayowezekana kupitia usimamizi makini na ujenzi wa miundombinu bora.