MRADI WA BANGULO WAWAKOSHA KAMATI YA SIASA ILALA

Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Ilala ya Chama cha Mapinduzi (CCM) chini ya Mwenyekiti wake, Mhe. Saidi Side wameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kwa usimamizi wa mradi wa maji Bangulo ambao upo hatua za mwisho za ukamilishaji wake ili uanze kuwahudumia wananchi.
Ametoa pongezi hizo baada ya kamati hiyo kufanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo Wilaya ya Ilala na kutembelea mradi huo uliohusisha ujenzi wa tanki kubwa la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita milioni tisa lililopo kata ya Pugu station.
"Nitoe pongezi kwa hatua hii iliyofikiwa ambayo tumeshuhudia sasa mradi tunaona upo asilimia 99 ya utekelezaji wake na siku chache zijazo wananchi wanufaika wataanza kupata huduma. Nikupongeze sana Mtendaji Mkuu wa DAWASA na watumishi wote kwa usimamizi mzuri wa fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 36 za utekelezaji wa mradi huu na sasa tunaona thamani yake," amesema Mh. Side
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uwekezaji mkubwa kwa wakazi wa Dar es salaam ya Kusini kupitia mradi wa Maji Bangulo na kupongeza ushirikiano mkubwa walioupata kama Serikali ya Wilaya kutoka kwa watendaji wa DAWASA katika kipindi chote cha utekelezaji.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire amesema kazi inayoendelea sasa ni kuanza kuyaruhusu maji kidogo kidogo kwenda katika mtandao wa DAWASA pamoja na kazi ya kusafisha mabomba kama hatua za awali za ukamilishaji mradi na kuanza kuhudumia Wananchi.
"Mradi wetu upo katika asilimia 99 ya utekelezaji, tumekwisha jaza tenki maji na tumeanza kuyaachia kidogo kidogo kwa nia ya kuyaingiza katika mtandao wa DAWASA pamoja na kusafisha mabomba na ndani ya siku chache mbele tunawahakimishia Wananchi wataanza kupata maji kupitia mradi huu," amesema Mhandisi Bwire.
Mradi wa maji Bangulo umetekelezwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 36 huku ukihusisha kazi za Ujenzi wa Tenki lenye ujazo wa lita milioni 9, Kituo cha Kusukuma Maji na Ulazaji wa bomba kwa umbali wa kilomita 119 na utahudumia wakazi wapatao 450,000 katika Kata za Mzinga, Kipunguni, Kitunda, Pugu station, Kiluvya, Msigani na Kinyerezi.