Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
MRADI WA BILIONI 1.82 WATEMBELEWA NA MWENGE UBUNGO, DAWASA YAPEWA KONGOLE
17 Apr, 2026
MRADI WA BILIONI 1.82 WATEMBELEWA NA MWENGE UBUNGO, DAWASA YAPEWA KONGOLE

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetakiwa kuhakikisha inakamilisha miradi ya maji kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika na huduma hiyo muhimu bila ucheleweshaji.

Rai hiyo imetolewa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, ndugu Wazo Mwang’onda, wakati Mwenge wa Uhuru ulipotembelea na kukagua mradi wa maji wa Msumi uliopo Kata ya Mbezi, Wilaya ya Ubungo. 

Akiwa katika ziara hiyo, ametoa pongezi kwa juhudi zinazofanywa na DAWASA katika kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi.

“Niwapongeze DAWASA kwa kazi nzuri ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji. Ni muhimu kuongeza nguvu katika utoaji wa huduma ili kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa ufanisi,” amesema ndugu Mwang’onda.

Amesisitiza kuwa kukamilika kwa miradi ya maji kwa wakati ni jambo la msingi katika kuhakikisha uwekezaji unaofanywa na Serikali unaleta matokeo chanya kwa wananchi, sambamba na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Albert Msando, ameishukuru Serikali kupitia DAWASA kwa kutambua changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Msumi na kuanzisha mradi huo wenye manufaa makubwa kwa jamii. 

Ameeleza kuwa maelekezo ya kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati yamepokelewa, na ataendelea kushirikiana na DAWASA ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa wananchi kama ilivyopangwa.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, amesema Mamlaka imepokea maelekezo hayo na inaendelea na juhudi za kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa inakamilika kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika kikamilifu.

Amefafanua kuwa mradi wa maji wa Msumi unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.82 kutoka Serikali, na unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba mwaka huu. 

Mradi huo unahusisha ulazaji wa mabomba yenye ukubwa wa kuanzia inchi 1.5 hadi 8, ujenzi wa kituo cha kusukuma maji, ujenzi wa kioski cha maji pamoja na ufungaji wa mfumo wa umeme.

“Mradi huu unalenga kuongeza upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa kiasi cha lita 2,160,000 kwa siku, na unatarajiwa kunufaisha takribani wakazi 18,000 wa eneo lote la Msumi,” ameeleza Mhandisi Bwire.

Kwa upande wake, mkazi wa Mtaa wa Msumi, ndugu Hamida Musa, ameipongeza Serikali kupitia DAWASA kwa juhudi zake za kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama, akieleza kuwa mradi huo utaleta nafuu kubwa kwa jamii mara tu utakapokamilika.

Kwa ujumla, mradi wa maji wa Msumi ni miongoni mwa miradi muhimu inayotekelezwa na Serikali kwa lengo la kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam, na unatarajiwa kuboresha hali ya maisha ya wananchi pamoja na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.