MRADI WA JAMII KIDUGALO WAKABIDHIWA RASMI DAWASA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeanza zoezi la kufunga mita kwa Wanachi waliokuwa wakihudumiwa na mradi wa maji wa jamii Kidugalo uliopo katika Kata ya Visiga eneo la Kibaha vijijini kwa lengo la kuboresha huduma baada ya mradi huo kukabidhiwa DAWASA mwaka 2023 kwa uendeshaji.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo Mhandisi wa miradi DAWASA-Mlandizi, Ally Migeyo amesema mradi huo ni mmoja wa miradi iliyochukuliwa na Mamlaka na juhudi za kuboreha huduma ya maji zinaendelea.
"DAWASA imepewa jukumu la kutoa huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, na kupitia mabadiliko ya Sheria ya Maji ya Mwaka 2019 kifungu namba 5, hivyo kutokana na sheria hiyo, Mamlaka ilianza taratibu za makabidhiano ya mradi huo uliokuwa ukiendeshwa na Wananchi kwenda DAWASA.
"Tulianza taratibu za makabidhiano ya usimamizi wa huduma ya maji mapema mwaka huu kwa kuwatambua wateja na kuwaingiza katika mfumo rasmi wa DAWASA. Zoezi linaloendelea sasa ni ufungaji wa mita za maji kwa wateja na kuhakiki zilizopo. Awali mradi ulikuwa na wateja 125 na baada ya kukabidhiwa una wateja 195”ameeleza Mhandisi Migeyo.
Bi. Fatuma Mongi, mmoja wa wanufaika wa mradi ameishukuru Serikali kupitia DAWASA kwa kuanza kutambulika rasmi kama mteja wa DAWASA na kutoa wito kwa huduma ya Maji kuboreshwa zaidi.
Mradi wa maji Kidugalo ni miongoni mwa miradi iliyokuwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA), na kukabidhiwa rasmi DAWASA kwa uendeshaji.